Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba wa Polisi aliyejinyonga mahabusu ataka uchunguzi

Kujinyongapic Data Askari Grayson Mahembe

Wed, 2 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati Jeshi la Polisi likieleza jinsi mkaguzi msaidizi wa polisi Grayson Mahembe alivyojinyonga akiwa mahabusu, hatua iliyoibua hisia na maswali kadhaa, baba mzazi wa marehemu Gaitan Mahembe, ameendelea kulitaka jeshi hilo kuweka wazi uchunguzi wa kifo cha mwanawe.

Mahembe alikuwa miongoni wa maofisa wa jeshi hilo wanaodaiwa kumnyang’anya Sh33.7 milioni mfanyabiashara wa madini Mussa Hamis, kisha kuutupa mwili wake vichakani huku katika kijiji cha Namgogoro mkoani Mtwara Januari 5, 2022.

Taarifa ya Polisi

Taarifa iliyotolewa Jumatatu na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema kuwa Grayson Mahembe aligundulika kujinyonga Januari 22, 2022 akiwa mahabusu kutokana na tuhuma za kumnyang’anya fedha na kisha kumuua Mussa Hamis na kuutupa mwili wake.

“Baada ya kufanya tukio hilo la ukiukwaji wa viapo vyao, akiwa na wenzake, wakiwamo maofisa, wakaguzi na askari wengine, hawakutoa taarifa kwa viongozi wao kwa sababu walifahamu kuwa wamefanya hivyo kwa nia ovu, kwa tamaa zao na kinyume cha sheria za nchi,” ilisema taarifa ya Misime.

Iliendelea kusema kuwa, baada taarifa za tukio hilo kuwafikia viongozi wa Polisi Mkoa wa Mtwara, walianza uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwakamata askari waliokuwa wanatuhumiwa.

“Miongoni mwa askari waliokamatwa na kuanza kuhojiwa ni huyo mkaguzi msaidizi wa Polisi Grayson Mahembe. Alipohojiwa alieleza mtiririko mzima wa matendo waliyofanya na mwisho akawapeleka maofisa waliokuwa wanafanya uchunguzi wa tukio hili sehemu walipoutupa mwili wa Mussa Hamis na maelezo yake yaliandikwa na yakawa yamerandana na ushahidi mwingine uliokuwa umekusanywa,” ilisema taarifa ya Misime.

Alisema baada ya hatua hiyo aliwekwa katika mahabusu ya peke yake kama walivyofanyiwa wenzake ambao taarifa inasema ilibidi wapelekwe mahabusu za Mkoa wa Lindi ili wasiharibu ushahidi uliokuwa ukiendelea kukusanywa. Ni maelezo yanayojibu swali marehemu aliwezaje kujinyonga akiwa mahabusu.

“Baadaye ndipo ikagundulika Grayson Mahembe amejinyonga. Baada ya tukio hilo taratibu zote za ukaguzi wa matukio zilifuatwa ikiwemo kupiga picha na zipo kwa kutumia wataalam wa kuchunguza matukio kama hayo’ ilisema ikiwa ni kujibu swali kuhusu picha za marehemu akiwa amejinyonga.

Alisema Mahembe asingeweza kuzikwa kijeshi kwa kuwa alipoteza sifa ya kufa kishujaa.

Familia yataka ripoti iwekwe wazi

Akizungumza kwa simu jana baada ya taarifa ya Polisi kutolewa, baba mzazi wa Grayson, alisema bado wanalitaka jeshi hilo kuweka wazi taarifa ya kifo cha mtoto wao.

“Postmoterm hatujapewa na mimi kinachoniuma zaidi ni kwamba, ndugu yangu alikuwepo kule kwa nini hakuitwa kwenda kushuhudia mtu aliyejitundika, kwa nini picha yeyote ya mtu aliyejitundika haikuonyeshwa, hiyo wamefafanua nini?” alihoji Mahembe.

Alimtaja ndugu yake aliyesema ni ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akisema walimtuma kufuatilia tukio hilo, lakini alipelekwa kuonyeshwa mwili ukiwa chumba cha maiti.

“Ninachosikitika ni kwamba amekwenda kuitwa kwenda kuona mwili wa marehemu Ligula hospitali basi, lakini sehemu ya tukio alipojinyongea hakuna anayejua,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa wamewatuma baadhi ya ndugu kuchukua vitu vya marehemu na kufuatilia zaidi.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia, Misime alisema hakuna aliyehitaji kuiona hiyo taarifa ya uchunguzi au picha kwa kufuata taratibu akanyimwa.

“Kama wanahitaji kuiona na kuona picha wafuate taratibu na siyo kama mmoja alivyosema hakuna picha iliyoonekana katika chombo chochote cha habari kwa maana kwamba alitaka zisambazwe kwenye vyombo vya habari wakati kufanya hivyo si sahihi na ni kinyume na sheria,” alisema.

Kuhusu mtu kujinyonga akiwa mahabusu, alisema: “Binadamu aliyekata tamaa ya maisha, mwenye msongo wa mawazo na anayefikiria aibu au adhabu atakayoipata kutoka na kile alichofanya, kama ameweka nia, hachagui eneo la kutimiza lengo lake, alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz