Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba na wanaye mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya ndugu yao

Mauaji Abc.jpeg Baba na wanaye mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya ndugu yao

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wanne wa familia moja, wakazi wa kijiji cha Munge, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kumuua ndugu yao, Simon Mollel (35) kwa kumchapa kwa fimbo.

Watu hao ambao ni baba mzazi wa marehemu na wanawe watatu, wanadaiwa kumchapa ndugu yao kwa fimbo na kusababisha kifo chake, ikiwa ni adhabu kutokana na kulewa pombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa leo Jumatano Oktoba 26, 2022, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa limetokea Oktoba 24, 2022 saa 2:47 asubuhi, katika Kijiji cha Munge.

Kamanda amewataja waliokamatwa kuwa ni Leshoo Kisoki Mollel (90) ambaye ni baba wa marehemu na wanawe Simon Leshoo Mollel (30) Baraka Leshoo Mollel (38) na Abedi Leshoo Mollel (15).

Kamanda Maigwa amesema siku ya tukio mwili wa marehemu ulikutwa katika nyumba ambayo ujenzi wake bado haujakamilika (pagala) ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mgongoni, baada ya kuchapwa fimbo na watuhumiwa hao na kusababisha kifo chake.

Alieleza kuwa, upelelezi wa awali umebaini kuwa Oktoba 24 saa 12:00 asubuhi watuhumiwa wakiongozwa na Leshoo Kisoki Mollel walifika nyumbani kwa marehemu na kumuita kwa ukali, wakimwambia kuwa amewaaibisha kwenye kikao walichofanya cha usuluhishi kwamba alikuwa amelewa pombe na hivyo anastahili adhabu.

"Walimchukua na kuondoka naye, kisha kumchapa kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na ndipo umauti ulimkuta. Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa daktari na kubaini chanzo cha kifo ni kuvunjika kwa bandama na pingili za mgongo vilivyosababishwa na kupigwa na kitu butu,"amesema Maigwa.

Aidha kamanda amesema upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta na kuwakamata wote waliohusika kwenye tukio hilo.

Kamanda ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuitaka jamii kuwatumia viongozi wa dini, serikali na jeshi la polisi, katika kushughulikia masuala ya kimaadili katika jamii kuliko kujichukulia sheria mkononi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live