Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe linaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika na mauaji ya Baba na mwanae yaliyotokea Desemba 12, 2023,katika kijiji cha Hangomba Kata ya Bara wilayani Mbozi ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Hayo yamebainishwa wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya, alipofika na kutoa pole kwa mama aliyepoteza mume na mtoto wake kutokana na tukio la mauaji hayo kijijini hapo.
Aidha, kamanda Mallya alitoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Naye Martine Mbembela, Mwenyekiti wa kijiji hicho kwa niaba ya mama huyo aliyepoteza familia yake alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuonesha ushirikiano na kufika kumpa pole mama huyo kutokana na familia yake kukumbwa na mkasa huo.