Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba, mama wadaiwa kutelekeza mtoto wa miaka miwili, DC awasaka

52905 MTOTO+PIC

Thu, 18 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Wakati duniani kuna watu wengi hawana watoto na miongoni mwao wamekuwa wakilazimika kuasili watoto wasiowazaa ili wawalee, upande mwingine wimbi la wazazi kutupa au kuwatelekeza watoto limeendelea.

Kwa hapa nchini wimbi la utupaji watoto limekuwapo licha ya Serikali na wadau mbalimbali kukemea na kuwasihi wazazi na walezi kuacha tabia hiyo.

Safari hii tukio la aina hiyo limetokea katika kitongoji cha Kangombe wilayani Malinyi mkoani hapa, ambapo mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili, Victoria, anadaiwa kutelekezwa na wazazi wake.

Kutokana na kutelekezwa kwa mtoto huyo, mkuu wa wilaya hiyo, Majura Kasika ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wazazi hao popote walipo ili wajibu tuhuma zinazowakabili.

Awali, akizungumza na Mwananchi juu ya mazingira aliyomkuta mtoto huyo, msaidizi wa Kituo cha Sheria Malinyi, Martha Elimba alisema akiwa katika shughuli za utoaji wa elimu ya jinsia na kisheria katika kitongoji hicho, alipata taarifa ya kuwepo kwa mtoto anayedaiwa kutelekezwa na wazazi wake kwa ndugu na kwamba, anaishi katika mazingira magumu.

“Nikiwa pale kitongojini walikuja akinamama na kunieleza kuwa kuna mtoto anaishi mazingira magumu, hivyo kuomba asaidiwe,” anasema Martha.

Anasema alifika katika nyumba anayoishi mtoto huyo na kumkuta akiwa amewekwa kando ya kichaka, nguo alizovaa zikiwa zimechakaa huku zikitoa harufu na mwili wake ulikuwa na kinyesi.

Martha anasema ngozi ya mtoto huyo ilikuwa imekakamaa.

Anasema Victoria anadaiwa kuachwa na mama yake nyumbani kwa dada wa mama huyo.

Juhudi za Mwananchi kumpata mama aliyeachiwa mtoto huyo kuzungumzia mazingira aliyoachiwa hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, Martha anasema kwa mujibu wa habari alizopewa ni kwamba, mzazi wa mtoto huyo aliondoka bila kusema anakokwenda na pasipo kuaga.

Anasema alimkuta mtoto huyo akiwa amedhoofika, na alivyoona hivyo alimtoa sehemu alipokuwa amewekwa na kumuogesha, kisha akaondoka naye hadi ofisi za Ustawi wa Jamii wilayani Malinyi.

Anasema ofisi hizo zilichangia kiasi cha Sh50,000 zilizotumika kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Misheni Lugala pamoja na kununulia mahitaji mengine.

Alivyopokewa hospitali

Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Misheni Lugala, Neema Kyelula anasema Victoria alipokewa Machi 25 akiwa na tatizo la utapiamlo uliopitiliza pamoja na uzito mdogo wa kilo tano ikilinganishwa na umri wake. Kwa umri wake alipaswa kuwa na uzito wa kati ya kilo kumi hadi kumi na mbili.

Kyelula anasema katika uchunguzi wa awali mtoto huyo alikutwa na malaria pamoja na upungufu wa damu, huku akiwa hawezi kutembea, miguu na mikono imekakamaa na ngozi yake ilikuwa kavu yenye mabaka na iliyokakamaa.

“Alivyofikishwa hapa ungeweza kusema ni mlemavu kutokana na kutokuwa na lishe nzuri kutokana na kuwa na utapiamlo uliopitiliza ambao hauwezi kumfanya mtoto wa aina hiyo kukua, kwa namna hiyo ni rahisi kupata magonjwa mengine,” anasema Kyelula.

Anasema kuwa baada ya kupimwa alianzishiwa matibabu na kuanza kupatiwa lishe, huku akipewa dawa ya kuongeza damu haraka.

Muuguzi huyo anasema hospitali imemuanzishia chakula dawa kwa ajili ya kumpatia protini ili kujenga mwili.

Pia kuna mlezi ambaye anajitolea kumlea mtoto huyo na ofisi ya mkuu wa wilaya imekuwa ikitoa fedha kusaidia mahitaji mengine kama mavazi na chakula.

DC awasaka wazazi

Mkuu wa wilaya ya Malinyi, Kasika anasema, “mama yake sasa atafutwe na kushtakiwa kwani jambo alilolifanya halikubaliki.”

Akiwa katika hospitali hiyo kumtembelea mtoto huyo, Kasika alisema uongozi wa wilaya hauwezi kuacha matukio ya utelekezaji watoto yaendelee, bali watahakikisha kuwa hatua zinachukuliwa kwa wazazi wanaofanya hivyo. Aliwasihi wananchi kujitokea kumsaidia mtoto huyo kwa kuwa bado anahitaji msaada.



Chanzo: mwananchi.co.tz