Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba bado amsaka mwanaye aliyetimiza siku 81

31977 Pic+mtoto TanzaniaWeb

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Idrissa Ally (13), aliyetekwa kwa staili ya kimafia ametimiza siku 81 bila kuonekana, lakini baba yake, Ally Idd bado ana matumaini ya kumuona akisema hatachoka kumtafuta hadi atakapompata akiwa hai au hata kuuona mwili wake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Idd alisema anaendelea na jitihada za kumtafuta mwanaye huyo wa kwanza kati ya wawili wa kiume alionao.

Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate alitekwa Septemba 26, saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Idrissa alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota IST, ambaye baada kuwafukuza marafiki wa mtoto huyo alimpulizia kitu kinachodhaniwa kuwa ni ‘spray’ kisha akamuingiza katika gari lake kupitia mlango wa nyuma.

Mzazi huyo alisema, “Nikiuona mwili wake nitasema nimechoka, lakini kwa sasa bado naendelea kumtafuta kwa kumtanguliza Mungu mbele maana najua yeye ndiye muweza wa yote.”

Alisema anashirikiana na polisi kumtafuta mtoto huyo na alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kutoa taarifa kwa vyombo vya dola endapo watamuona.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema hawajapata taarifa zozote kuhusu mtoto huyo. “Bado tunaendelea na upelelezi, endapo tukizipata taarifa zozote tutauambia umma,” alisema Mambosasa.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Princes Gate, Mussa Idrissa alisema wamefunga shule, lakini mtoto huyo alikosa mitihani ya majaribio na ile ya mwaka ambayo ingemwezesha kuingia darasa la sita mwakani.



Chanzo: mwananchi.co.tz