Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba aua binti zake wawili, ajinyonga

17582 Pic+baba TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, Dotusi Isaya anadaiwa kuwaua watoto wake wawili, kumjeruhi kwa panga mkewe pamoja na mama mkwe, kisha kujiua.

Akizungumzia tukio hilo jana, kamanda wa polisi Mkoa wa Lindi, Pudensiana Protas alisema Isaya alifanya mauaji hayo usiku wa kuamkia jana huko Nachingwea mkoani humo.

Kamanda Protas alisema mtuhumiwa alikwenda Nachingwea anakoishi mkewe Mariam Lucas na kujificha pembeni mwa nyumba ambayo haijamaliza kujengwa (pagala) akimvizia kisha kumkata panga eneo la kisogo na begani.

“Baada ya kumkata mkewe aliingia ndani ya nyumba (katika) chumba wanacholala watoto na kukuta wanawe wawili wamelala na watoto wengine, lakini yeye aliwaua wanawe kwa kuwakatakata,” alisema kamanda huyo.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Clara Dotusi (5) na Herieth Dotusi (3).

Kamanda alisema baada ya mtuhumiwa kutekeleza unyama huo aliingia chumbani kwa mkewe na kujinyonga kwa kutumia kanga.

Alisema Mariam amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri, huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mkwe azungumza

Akizungumzia tukio hilo, mama mzazi wa Mariam, Amanda Joseph alisema mauaji ya wajukuu zake yalitekelezwa na baba yao baada ya kumtishia maisha mkewe kwa muda mrefu.

Amanda alisema Isaya aliamua kufanya tukio hilo baada ya mkewe kumkatalia asiende na watoto wake Bukoba baada ya kuondoka jijini Dar es Salaam walikokuwa wakiishi awali.

“Mimi mwenyewe alinipiga panga, basi katika kukimbia wakabaki watoto na baada ya kumaliza mauaji hayo akajinyonga,” alisema.

Akisimulia zaidi, alisema bintiye aliamua kuondoka kwa mumewe jijini Dar es Salaam baada ya kuchoshwa na maisha magumu.

Alisema Mariam alimwambia mume wake kuwa watoto wakiwa wakubwa atawachukua, lakini kwa sasa ataendelea kuishi nao kwa kuwa bado ni wadogo.

Amanda alisema Isaya alipofika Nachingwea alimuuliza mkewe sababu za kuondoka Dar es Salaam iwapo ni suala la ugumu wa maisha au alikuwa amepata mwanaume mwingine.

“(Isaya) akamwambia basi nitakuwashia moto na ilipofika juzi, akamwambia kama hunitaki mimi naenda kufa leo. Ndipo saa tano usiku alipokuja kutekeleza mauaji hayo.”

Mganga, mashuhuda

Mganga mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Dk Laizer Samwel alisema majeruhi alipokewa katika hospitali ya wilaya akiwa hana fahamu na sasa ameanza kupata fahamu.

“Mgonjwa sasa anaendelea vizuri, aliletwa akiwa hana fahamu na analalamika maumivu baada ya kupata ufahamu,” alisema Dk Samwel.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nambambo Mazoezi, Aron Banda alisema kuna sehemu ulifanyika uzembe kwa kuwa Mariam alitoa taarifa polisi za kutishiwa maisha na mumewe.

“Nimepata taarifa ambazo sijazithibitisha sana kwamba huyu mama ambaye amejeruhiwa alitoa taarifa kituo cha polisi, lakini jana hiyohiyo tukio limetokea saa tano,” alisema Banda.

Alisema iwapo polisi wangefanyia kazi taarifa yake wangeweka ulinzi kwa sababu muuaji alifanya mauaji hayo saa tano usiku.

Shuhuda wa tukio hilo, Ashura Lipala alisema walianza kusikia vilio saa sita usiku na walipofika eneo la tukio waliwakuta majeruhi wawili (Amanda na Mariam) pamoja na maiti za watoto wawili.

“Tuliingia ndani tukakuta watoto wawili wamekatwa mapanga vibaya, kibaya zaidi polisi walipofika wakakuta baba yao amejinyonga,” alisema Lipala.

Mtazamo kisaikolojia

Mwanasaikolojia, Charles Nduku alieleza kuwa hadi mtu anafikia hatua ya kujiua kuna mkusanyiko wa mambo mengi ikiwamo maumivu, hasira na kutoridhishwa na hali ya maisha au hata ndugu na marafiki.

Alisema wanaume ndio wanaongoza kwa kufanya uamuzi wa kujiua ikilinganishwa na wanawake kutokana na tofauti za kibaiolojia.

“Wanaume ndio wanaongoza kwa kujiua sana kuliko wanawake kwa sababu wanaume tunabeba hasira kwa haraka, lakini wanawake wana uwezo wa ku-hold (kuvumilia) maumivu kwa muda mrefu,” alisema Nduku.

Alisema jambo jingine ni kwamba wanaume si wepesi kueleza matatizo yao kwa watu wengi tofauti na wanawake ambao wanaweza kuelezena matatizo wao kwa wao.

“Wanawake wana-share (wanashirikishana) pale wanapokuwa na matatizo na kushare tatizo ni nusu ya kulitatua,” alieleza.

Alitaja sababu za kujiua ikiwamo hali ngumu ya maisha, matatizo ya kiakili kama msongo wa mawazo (depression) pamoja na wivu wa kimapenzi hasa kwenye ndoa.

“Inatokea mtu amefiwa na mke wake anapata msongo wa mawazo na anajiona hatakiwi kuishi duniani,” alisema Nduku.

Alisema, “mwisho wa siku watu waliojiua wanajisikia hawana umuhimu duniani, hakuna mtu anayempenda hivyo anaona hana umuhimu. Endapo ungekutana na mtu huyo siku moja kabla na ukamwambia nakupenda sana anaweza asijiue.”

Matukio ya mauaji

Hilo si tukio la kwanza la mzazi kuua watoto wake kwani Aprili 2017, mkazi wa Bukoba, Respicius Deogratius aliwaua wanawe mapacha waitwao Nyakato na Nyangoma kwa kuwakata vichwa.

Tukio jingine ni la Aprili mwaka huu ambapo Pius Salum, mkazi wa Matai, Kalambo mkoani Rukwa alimuua mtoto wake, Benedicto Salum (13) kwa kumpiga ngumi na mateke tumboni akidai si wake.

Kwingineko duniani, mkazi wa Carolina nchini Marekani, Timoth Ray Jones aliwaua watoto wake watano kwa kuwanyonga baada ya kutengana na mkewe mnamo Julai.

Agosti mwaka huu, mkazi wa Colorado nchini humo, Christopher Watt aliwaua mabinti zake wawili na mkewe. Miili ya watu hao ilikutwa imezikwa karibu na makazi yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz