Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba atupwa jela maisha kwa kumnajisi mwanaye gesti

Screenshot 20221029 085444 Opera News Baba atupwa jela maisha kwa kumnajisi mwanaye gesti

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imemhukumu kifungo cha maisha jela Alphonce Ngassa, maarufu kama Dutwa (51) kwa kumnajisi mtoto wake wa kike mwenye miaka tisa (jina limehifadhiwa).

Mshtakiwa huyo alihukumiwa kifungo hicho baada ya kutiwa hatiani kwa kumweka binti yake katika nyumba ya kulala wageni na kumfanyia vitendo hivyo mwezi mzima huku akimziba mdomo asipige kelele.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Mpuya, alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo mwishoni mwa mwaka jana.

Hakimu Mpuya alisema mashahidi sita, akiwamo mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho, walitoa ushahidi katika mahakama hiyo.

Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alisema mahakama imejiridhisha pasipo kuacha shaka kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo, hivyo kumtia hatiani.

Mahakama hiyo ilielezwa kuwa, mshtakiwa huyo alimchukua binti yake huyo kutoka Kahama mkoani Shinyanga alikokuwa anaishi na mama yake mzazi ambaye walitengana na kwenda naye Jijini Mwanza kwa ahadi ya kwenda kumnunulia viatu vya kanisani.

Aidha, ilidaiwa kuwa ahadi hiyo haikutekelezwa na mshtakiwa badala yake alimpeleka kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kuanza kumfanyia vitendo hivyo.

Taarifa za mtoto huyo kufanyiwa unyama huo zilitolewa na mtu aliyejulikana kwa jina la Minja, ambaye alibaini mwenendo wa mtoto huyo haukuwa sawa na kuanza kumdadisi ndipo akamwambia kuwa baba yake mzazi alikuwa akimfanyia vitendo hivyo.

Minja alidai katika mahojiano, mtoto huyo alikiri kufanyiwa vitendo hivyo, huku akidai baba yake alikuwa akimziba mdomo wakati akimnajisi ili asipige kelele.

Kutokana na hali hiyo, Minja alimpeleka mtoto huyo kituo cha polisi na kufungua kesi namba 162 ya mwaka 2021 ya ubakaji na kupewa fomu namba 3 ya polisi kisha akampeleka hospitalini.

Majibu ya daktari aliyemfanyia vipimo yalionyesha kuwa binti huyo aliingiliwa mara nyingi na sehemu zake za siri zilikuwa katika hali mbaya.

Daktari aliyempima alitoa ushahidi wake mahakamani hapo ikiwamo kuwasilisha fomu hiyo namba tatu ya polisi kama kielelezo.

Baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wote uliotolewa na mashahidi sita akiwamo mtoto mwenyewe, ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kutokana na shtaka linalomkabili, lakini alikataa kujitetea.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ghati Mathayo, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na kufanya kitendo kibaya dhidi ya mtoto wake wa kumzaa ambaye ni mdogo na kumharibu sehemu zake za siri, na kumharibu kisaikolojia kwa kumnajisi mwezi mzima.

Kutokana na ushahidi pamoja na maelezo ya mwendesha mashtaka, mahakama ilimhukumu kifungo cha maisha jela.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live