Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba atoa ushahidi kortini kuhusu kifo cha mwanawe

Sheria Ya Uganda Dhidi Ya Wapenzi Wa Jinsia Moja Yapingwa Mahakamani Baba atoa ushahidi kortini kuhusu kifo cha mwanawe

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfanyabiashara Lumumbu Mtui anayejihusisha na usafirishaji mizigo na umiliki wa maroli, amedai mahakamani kuwa alipokea ujumbe kutoka kwenye simu ya marehemu mtoto wake, Jonson Mtui kwamba kutokana na kiburi cha mwanawe, kimemponza na aanzie Chalinze.

Alidai kuwa ujumbe ulimfanya apige simu kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kondoa kuhusiana na ujumbe huo, akimweleza kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Chalinze anadai wamekuta gari porini na ndani kuna mwili wa Jonson Mtui na mwili wake wakati huo ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mlandizi.

Mtui alidai hayo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Jaji Hussein Mtembwa.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Ditrick Mapunda, shahidi huyo alidai mtoto wake alikuwa anaendesha gari aina ya Scania na walikuwa wanafanya kazi ya kusafirisha mizigo.

Alidai kuwa Aprili 29, 2020, akiwa nyumbani kwake Kondoa, alifika mtoto wake Jonson akiwa pamoja na tandiboi wake, Edward Nyagawa na kumwambia kwamba wamepata mzigo wa mbao Mafinga, wanakwenda kupakia na kupeleka Dar es Salaam.

Shahidi huyo alidai kuwa aliwaruhusu kwenda kupakia mzigo huo na alikuwa anawasiliana nao kujua kama wamefika, alikuwa anawasaliana na Jonson na muda ambao alikuwa hampati, alimpigia tandiboi wake Edward.

Mtui alidai kuwa Mei 21, 2020, alimpigigia simu Jonson ili ampe mzigo wa saruji kutoka Dar es Salaam warudi nao Kondoa, simu hazikupokewa ikiwamo ya tandiboi wake ambayo iliita pasi na kupokewa.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya muda, alipokea ujumbe ukisema "kutokana na kiburi cha mwanao si kiburi kutenda, mwanao kiburi kimemponza, anza na Chalinze". Ujumbe huo ulitumwa kupitia namba ya simu ya mwanawe.

"Nilikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kondoa, nilionesha ujumbe, Mkuu wa Kituo kule Kondoa, alipiga simu Kituo cha Polisi Chalinze, baadaye akamwambia kuwa wamekuta gari porini na ndani kuna mwili wa Jonson Mtuli na mwili wake ulikuwa umehifadhiwa Hospitali ya Mlandizi.

Mtui alidai aliwasiliana na vijana wake wa Dar es Salaam, akiwamo Allen Mtui, wafuatilie mwili na baada ya kuupata ulipelekwa Moshi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.

"Huyo tandiboi siku hiyo hakupokea simu yangu, kwenye mazishi hakukanyaga hadi leo (jana) hii nimesimama hapa mahakamani ndipo ninamwona, yule pale, ninaamini yeye ndiye amehusika na kifo cha mwanangu," alidai.

Daktari Sudi Msakamali kutoka Hospitali ya Msiga, alidai alifanya uchunguzi wa mwili wa Jonson, kipindi hicho alikuwa anafanya kazi Kituo cha Afya Chalinze kama Daktari Mfawidhi.

Alidai kuwa Mei 21, 2020, alifuatwa na polisi kituoni huko kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwili huo. Baada ya uchunguzi alibaini kifo cha Jonson kilisababishwa na kuvuja damu nyingi.

Pia alidai mwili huo ulikuwa na majeraha kichwani, sehemu ya nyuma na katika paji la uso lenye upana na urefu unaokadiriwa sentimeta 3.3 kichwani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live