Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba aeleza mazito mauaji ya mwanaye

50571 Pic+baba

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jackson Makundi, baba mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Scolastica, Humphrey Makundi (16) aliyeuawa mwaka 2017, ameeleza namna alivyoutambua mwili wa mwanaye baada ya kufukuliwa.

Shahidi huyo alieleza pia kuwa mmoja wa wanafunzi aliyekuwa akisoma na mwanaye alimsisitizia afuatilie tetesi kuwa kuna mwanafunzi alipigwa na kuumizwa nyuma ya ukuta wa shule.

Mwanaye aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika shule hiyo, alitoweka shuleni hapo Novemba 6, 2017 na baadaye mwili wake ulibainika kuzikwa na Manispaa ya Moshi kwa madai ya kutotambuliwa.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wananchi ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, inasikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na Jaji Firmin Matogolo.

Akitoa ushahidi wake jana kama shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Makundi alidai Novemba 17, 2017 walifanikiwa kupata amri ya mahakama ya kuufukua mwili huo ukiwa umekaa kaburini kwa siku sita.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande, Makundi alianza kwa kueleza namna alivyopigiwa simu na mkuu wa shule hiyo Novemba 8, 2017 akimjulisha kutoweka kwa mwanaye.

Alidai kuwa alisafiri kutoka Dodoma hadi shuleni na kufanya mazungumzo na uongozi wa shule akiwamo Elizabeth Shayo mkurugenzi wa shule hiyo, mshtakiwa wa tatu Laban Nabiswa na wanafunzi.

“Walinihakikishia mtoto wangu angepatikana nivute subira. Baada ya kutopata majibu ya kuridhisha nilionana na mmiliki (Edward) akaniambia niondoe hofu asilimia 100 mtoto wangu angepatikana,” alisema mzazi huyo.

“Niliingiwa hofu kutokana na majibu yao. Niliomba kuonana na marafiki zake mwanangu ambapo nilionana nao mmoja alikuwa anaitwa Abdul, Edson na mwingine wa tatu.” “Niliwauliza nini kilichotokea kwa rafiki yao, walinieleza aliondoka shuleni hapo akiwa amevaa bukta, Tshirt na soksi lakini hakurudi tena,” alidai shahidi huyo ambaye ni mfanyabiashara jijini Dodoma.

Alidai kuwa Abdul alimweleza kuna tetesi kwamba mwanafunzi alipigwa na kuumizwa nyuma ya ukuta wa shule na alimsisitizia kuwa afuatilie jambo hilo.

“Watoto walinishauri kwa uchungu sana, nifuatilie jambo hilo maana rafiki yao aliondoka shuleni kwa mazingira ya kutatanisha, nilienda polisi kuomba kufuatilia mwili ule kama ni wa mwanangu ama la.”

Shahidi huyo alidai baada ya kuelezwa hivyo alikwenda Kituo cha Polisi Himo ambao walimthibitishia kuopolewa kwa mwili huo katika mto Ghona Novemba 10, 2017 na kupelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.

Hata hivyo alidai kuwa alifika Mawenzi na kukuta mwili huo ukiwa tayari umeshazikwa Novemba 12, hivyo ukafanyika utaratibu wa kuomba kibali cha Mahakama ili ufukuliwe.

Baada ya mwili huo kufukuliwa alidai kuutambua kuwa ni wa mwanaye kutokana na mavazi pamoja na jino lake moja ambalo lilikuwa limevunjika.

“Baada ya kumwagiwa maji mwili Mungu alivyo mkubwa niliona lile jino la mwanangu ambalo ndilo lililonifanya nimtambue, basi mwili ulichukuliwa na kupelekwa hospitali ya KCMC kwa ajili ya taratibu za uchunguzi.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wengi wa ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, inamkabili mmiliki wa shule hiyo Edward Shayo, mwalimu wa nidhamu Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janeth Joseph na Florah Temba, Moshi



Chanzo: mwananchi.co.tz