Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Auawa kwa kuchomwa kisu akiporwa simu

KAMANDA DSM Kamanda Muliro Jumanne Muliro

Fri, 7 Oct 2022 Chanzo: Ippmedia

Mkazi wa Mwananyamala, Manjunju mkoani Dar es Salaam, Billal Hoza (21), amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kundi la vijana waliomchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili na kumpora simu.

Vijana hao wapatao watano walimvamia kijana huyo aliyekuwa amekaa nje ya nyumba yao na kumchoma kisu mgongoni, upande wa moyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi saa 3:30 usiku, wakati Hiza na rafiki yake wakiwa wamekaa barazani nyumbani kwao, wakichezea simu.

“Wakati wanachezea simu walipita vijana kama wanne, kati yao mmoja akamfuata huyu kijana (Hoza) akampokonya simu, akaendelea kutembea na wenzake, ndipo Hoza akamfuata, akambana na kumtupa chini na mmoja wao akatoa kisu na kumchoma mgongoni, wakaendelea kutembea.”

MAMA MKUBWA ASIMULIA

Akisimulia kuhusu tukio hilo, mama mkubwa wa kijana huyo, Zabibu Maneno, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa tatu usiku wakati Hoza na rafiki yake Abrahamu Michael, wakiwa wamekaa barazani nje ya nyumba yao.

Alisema ghafla lilifika kundi la vijana wapatao watano na kutaka simu.

“Hoza alikuwa ameshika simu mkononi anaichezea, hawa wahalifu walipofika wakawa wanataka wapewe simu, rafiki wa Hoza alifanikiwa kukimbia, wamemchoma Hoza na kitu chenye ncha kali karibu na moyo, wamempora simu na kuondoka,” alisema.

RAFIKI AELEZA

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni rafiki wa marehemu, Abrahamu Michael, alisema baada ya kundi hilo kuwavamia, alifanikiwa kukimbia kwenda kutafuta msaada kwa majirani.

“Nilipokwenda kwa majirani kuomba msaada sikupata ushirikiano, niliporudi nikamkuta rafiki yangu akiwa amelala chini anatokwa damu, nilipiga kelele kuomba msaada sikupata, watu walikuwa wanamshangaa tu.

“Niliamua kumbeba hadi hospitali ya Mwananyamala, nikaambiwa tayari ameshafariki dunia,” alisema.

HOSPITALI

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala, Rajabu Kaseke, alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa Hoza.

Alisema waliupokea ukiwa na jeraha na jana ulichukuliwa na polisi kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ili kuchunguza ni jeraha la aina gani.

Chanzo: Ippmedia