Muleba. Mwanaume mmoja wa Kisiwa cha Ikuza wilayani Muleba amefariki na mwanamke mmoja kujeruhiwa baada ya kuchomwa visu sehemu tofauti za miili yao.
Diwani wa Kata ya Ikuza, Fortunatus Matha amemtaja aliyeuawa kuwa ni Masele Kalakiza (40) na aliyejeruhiwa ni Levina Gasper (38) ambaye amepelekwa katika Zahanati ya Kasenyi iliyopo kwenye kata hiyo.
Matha amesema tukio hilo limetokea jana, Septemba 23,2018 saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Nyakaralo kilichopo Kijiji cha Ikuza eneo la Msenyi chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.
"Mwanaume huyo ni mjasiriamali wa Kijiji cha Musonga kilichopo Kata ya Lunzewe wilayani Bukombe ameuawa na mkewe, Maria Masele (28) kutokana na wivu wa mapenzi," amesema Matha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuza, Lucas Kiberit amesema Maria alimfumania mume wake kichakani na kumchoma kisu upande wa kulia na utumbo kumwagika nje kabla ya kupoteza maisha.
Baada ya mauaji hayo, amesema Maria alikamatwa na uongozi wa kijiji na kukabidhiwa kwa askari wa kituo kidogo cha polisi kilichopo katika kisiwa jirani cha Kyakazimbwe ambao walimpeleka Kituo cha Polisi wilayani Muleba.
"Walikuwa kwenye starehe wanakunywa pombe ndipo mwanaume akachepuka kichakani na mwanamke mwingine ndipo mkewe akamfuata kisha kumchoma kisu na kumjeruhi mwanamke aliyekuwa naye," amesema Kiberiti.
Mwenyekiti huyo amewashauri wananchi kulinda na kuthamini ndoa na familia zao kwa kuepuka kujichukulia sheria mkononi na inapotokea basi wapeleke mashauir yao kwenye mamlaka husika.
Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Kasenyi inayomilikiwa na Kanisa la ELCT, Dk Martin Lujimya amesema majeruhi aliyejeruhiwa mkono wa kushoto ameshonwa majeraha yake na anaendelea na matibabu.
Mkuu wa kituo kidogo cha polisi cha Kyakazimbwe (OCS), Silasi Jeremiah amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa na baada ya kuhojiwa atafikishwa mahakamani.