Mkazi wa Kijiji cha Mgombani, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Juma Ndaji (27), anashikiliwa na polisi wilayani humo kwa kosa la kumkata panga mfanyabiashara, Paulo Akwesso (58) na kumsababishia kifo chake, akimtuhumu kuwa na uhusiano na mpenzi wake.
Mtuhumiwa huyo pia inadaiwa alimjeruhi kwa panga Rebeka John (22), anayesadikiwa kuwa ni mpenzi wake, ambaye amelazwa Kituo cha Afya Mto wa Mbu kwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne usiku Kitongoji cha Kirurumo, Kata ya Majengo, kwenye chumba cha mwanamke huyo.
Akifafanua chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa, kumtuhumu marehemu kuwa na uhusiano na mpenzi wake, ambaye pia alijeruhiwa kwa panga baada ya kuwakuta chumbani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Migombani, Festo Philpo alisema mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo alifika katika chumba cha Rebeka na kukuta polisi wakimhoji mtuhumiwa, ambaye alikiri kuhusika kumshambulia marehemu na kumsababishia umauti.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa marehemu alikuwa akifanya biashara ya kuuza vinywaji, huku Rebeca akiwa mfanyakazi wake.
Alisema awali mtuhumiwa alikuwa na uhusiano na Rebeca, lakini walitengana kitambo, hivyo hatua ya kuwenda kuwashambulia kwa panga ni kutokana na wivu wa mapenzi.
Alisema mtuhumiwa alipata taarifa kuwa marehemu amekuwa akienda katika chumba cha Rebeka na kulala, ndipo alipoamua kumvizia usiku akiwa na panga mkononi.
"Mtuhumiwa alifika katika chumba cha Rebeka na kumkuta marehemu akiwa chumbani na kuanza kumkata na panga na kuwajeruhi wote wawil, lakini marehemu Paulo alivuja damu nyingi sana na kufariki dunia, akipatiwa matibabu katika kituo cha afya Mto wa Mbu, '' alisema.