Mahakama ya wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, imemhukumu miaka 30 jela Emmanuel Masawe (50) mkazi wa Kigamboni mkoani humo kwa kosa la kumbaka binti wa kazi wa miaka (15) kwa nguvu, baada ya kumdanganya atampa taiti na kitenge ambavyo hata hivyo baada ya kumbaka hakumpa vitu hivyo.
Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Kiteto Mossy Sasi, alisema mahakamani hapo kuwa, hukumu hiyo imezingatia kukithiri kwa vitendo vya ukatili haswa ubakaji kwa watoto wadogo, hivyo ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo hicho cha miaka 30 jela.
Hakimu Sasi alieleza mahakamani hapo kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 23, 2021 majira ya saa 3:00 asubuhi nyumbani kwa Joyce Msiba mkazi wa eneo hilo la Kigamboni Kata ya Patimbo.
Alisema siku hiyo mtuhumiwa alifika nyumbani kwa jirani yake huyo akiwa na kitenge na nguo moja ya ndani vilivyofungwa kwa pamoja.
Hapo alimkuta binti huyo wa kazi ambaye jina lake limehifadhiwa aliyekuwa anamlea mtoto mdogo wa mwenye nyumba, na alianza kumdanganya na zawadi hizo ili afanye naye mapenzi.
Hakimu Sasi aliendelea kueleza mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa aliamua kumtoa mtoto mdogo anayekuwa analelewa na binti huyo nje ili iwe rahisi kwake kufanya naye mapenzi ambapo pamoja na kukataliwa zawadi hizo na binti huyo mtuhumiwa alitumia nguvu na kumbaka hapo ndani na kisha kuondoka.
Baada ya binti huyo kuachiwa alitoka na kuanza kuhaha kumtafuta mtoto huyo mdogo aliyetelekezwa nje ambapo hapo alikutana na majirani na kuwaeleza tukio hilo.
Mtuhumiwa aliposomewa shtaka lake hilo yeye alikana na kwamba alisema anasingiziwa hivyo atakuwa na shahidi mmoja huku upande wa mashtaka ukiwa na mashahidi nane.
Hivyo alimtaka aeleze mahakama kama ana cha kujitetea ili mahakama isimpe adhabu kali na kusema yeye anategemewa na mke na watoto hivyo Hakimu ampunguzie adhabu.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Joseph James mahakamani hapo alimweleza Hakimu kuwa mtuhumiwa, Emmanuel Masawe alitenda kosa hilo la ubakaji chini ya kifungu cha 130 (1) (2) (e) na Kif cha 131 (1) sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.