Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atupwa jela maisha kwa kusafirisha dawa za kulevya

Madawa Ya Kulevya Atupwa jela maisha kwa kusafirisha dawa za kulevya

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, masjala ndogo ya Mbeya, imemhukumu Keneth Mwamwaja kifungo cha maisha jela, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 248.91.

Hukumu hiyo ilitolewa hivi karibuni na Jaji wa mahakama hiyo, Yose Mlyambina baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha mashataka dhidi ya Mwamwaja pasipo kuacha shaka yoyote.

Sambamba na hukumu hiyo, mahakama iliagiza kuteketezwa kwa dawa hizo zilizokamatwa wakati wa upekuzi nyumbani kwa mshtakiwa.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi watano na vielelezo sita na upande wa utetezi walipeleka mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa bila kielelezo chochote.

Akisoma huku hiyo, Jaji Mlyambina alisema hukumu hiyo ilizingatia hoja za majumuisho za pande zote pamoja na maombi ya upande wa utetezi ikiwa ni pamoja na kudai kuwa mshtakiwa alikuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza, aliwekwa mahabusu kwa miaka zaidi ya minne, ni kijana mdogo wa miaka 37 na nguvu kazi ya taifa, pia ana familia inamtegemea.

“Nimefikiria kwa uchungu majumuisho ya pande zote na maombi ya upande wa utetezi, pia nimepitia vifungu vya sheria ya udhibiti wa za dawa za kulevya ambayo inaelekeza kuwa mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya atahukumiwa kifungo cha maisha,” alisema.

Alisema ni wajibu wa nchi kuhakikisha inakabiliana na makosa ya dawa za kulevya, hivyo sheria inabaki kuwa ndiyo mhimili mkuu wa kukabilia na makosa hayo.

“Katika hali hiyo ninamhukumu mshtakiwa Mwamwaja kwenda jela maisha kuanzia Februari 6, 2023 kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kama sheria inavyoamuru,” alisema.

Wakati wa kusikilizwa kesi ilidaiwa kuwa Juni 2, 2019 katika eneo la Jakaranda B mkoani Mbeya, mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa hizo za kulevya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live