Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atupa kichanga cha siku moja na kujisalimisha polisi

47802 Kichanga+pic

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanamke mmoja mkazi wa mtaa wa Kisiwani, Tabata Wilaya ya Ilala, Grace Peter anashikiliwa kwa kosa la kutupa mtoto wa siku moja kwenye karo la maji machafu na kisha kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi.

Mtoto huyo wa kiume aliokotwa jana akiwa amewekwa kwenye mfuko wa rangi ya chungwa na alipelekwa katika zahanati ya Kisiwani iliyopo mtaani hapo ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kuhamishiwa katika Hospitali ya Amana.

Akizungumza na mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala, Zuberi Chembera alisema baada ya kumhoji mzazi huyo alisema amechukua hatua hiyo kwa kuwa yupo peke yake hivyo asingeweza kumlea.

Ofisa mtendaji wa mtaa huo, Jane Kazimoto alisema taarifa za kuokotwa kwa mtoto huyo walizipata saa 3:45 asubuhi kutoka kwa majirani wa mama huyo.

“Baada ya kupata taarifa, tulifika eneo la tukio na kushuhudia mtoto huyo akiwa amefungwa kwenye mfuko. Tulimpeleka katika zahanati yetu ya Kisiwani lakini daktari alishauri apelekwe Amana,” alisema.

Kiongozi huyo wa mtaa aliwataka wanawake kuacha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Mkazi wa mtaa huo, Saumu Mkinga ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kubaini kuwa kichanga hicho kimetupwa alisema, wakati akiwa anaosha vyombo alisikia mtoto akilia lakini hakujali kwani alijua ni wa jirani yake.

“Lakini baada ya kuona mtoto huyo anazidi kulia nilitoka kwenda kwa jirani kuuliza lakini wakasema sio mtoto wao, ikabidi sasa nizunguke nyuma ya nyumba maana sauti ilitokea huko,” alisema na kuongeza:

“Nilipofika nilisimama kusikiliza sauti ya mtoto inatokea wapi kumbe yule mtoto alikuwa kwenye karo baada ya kufunua nikakuta mfuko nikaufungua kumbe ni mtoto, sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuita majirani,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz