Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atuhumiwa kwa ushahidi wa uongo, apanda kizimbani

45615 Pic+kizimbani Atuhumiwa kwa ushahidi wa uongo, apanda kizimbani

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkazi wa Ilala Shamba, Selemani Ndagala (58) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kwa mashtaka matano ya kutoa ushahidi wa uongo katika Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi.

Wakili wa Serikali, Janeth Magohe akisoma hati ya mashtaka mbele ya ya Hakimu Mkazi, Augustino Rwezile, alidai kuwa mshtakiwa huyo alitoa ushahidi wa uongo katika kesi ya dawa za kulevya inayowakabili Remy Sipuka na Amina Juma.

Magohe alidai kuwa katika shtaka la kwanza Februari 25, 2019 akiwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi akiwa shahidi wa kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2018 inayowakabili Remy Sipuka na Amina Juma, mshtakiwa alitoa ushahidi wa uongo kwa kueleza kwamba Amina na ofisa wa dawa za kulevya alimpigia simu akimfahamisha kuhusu upekuzi uliokuwa unakusudiwa kufanyika katika nyumba ya Sipuka, ushahidi ambao ni kinyume na ule alioandika katika maelezo yake uliorekodiwa na Ofisa Mkaguzi, Wamba Oktoba 6, 2017.

Katika shtaka la pili Februari 25, 2019 mshtakiwa akiwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi akiwa anajua alitoa ushahidi wa uongo akisema alimkuta Sipuka nyumbani kwake pasipo kumkuta Amina ambaye alikuja naye huku akijua ni kinyume na ule alioandika katika maelezo yake uliorekodiwa na Ofisa Mkaguzi, Wamba Oktoba 6,2017.

Katika shtaka la nne, Februari 25, 2019 akiwa Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi mshtakiwa alitoa ushahidi wa uongo akidai kuwa hakuona poda inayodhaniwa ni dawa za kulevya wakati wa upekuzi katika chumba cha Sipuka, kinyume na ule alioandika katika maelezo yaliyorekodiwa na ofisa mkaguzi, Wamba Oktoba 6, 2017.

Shtaka la tano Februari 25,2019 akiwa Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi, mshtakiwa akiwa shahidi alitoa ushahidi wa uongo na kudai kuwa hakuwahi kusaini maelezo wakati ofisa mkaguzi, Wamba alipomhoji Oktoba 6, 2017.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana makosa yanayomkabili. Wakili Magohe alidai kuwa upelelezi umekamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).

Hakimu Rwezile alisema dhamana ipo wazi na mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5milioni kwa kiloa mmoja.

Rwezile aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 20 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.



Chanzo: mwananchi.co.tz