Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atuhumiwa kutoa hongo dola 2,000

27561 Hongo+pic TanzaniaWeb

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi/Iringa. Mfanyabiashara mwenye asili ya India, Suresh Babu Kakolu Hongo amefikishwa mahakamani mjini hapa akidaiwa kutaka kutoa hongo ya dola 2,000 za Kimarekani kwa kigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mujibu wa mashtaka, Kakolu alitaka kutoa fedha hizo ambazo ni sawa na takribani Sh4.5 milioni za Kitanzania ili apate msamaha wa kodi ya Sh6.6 bilioni aliyolimbikiza tangu mwaka 2013.

Kakolu, anayemiliki hati ya kusafiria ya Uganda, alifikishwa Mahakama ya Wilaya Moshi, akituhumiwa kutaka kumhonga meneja wa TRA wa mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo.

Mshtakiwa huyo ni meneja wa fedha wa kampuni za ujenzi za Dott Services (TZ) Ltd na General Nile Company for Roads and Bridges na Dott Services JV.

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Rehema Mteta alimsomea Kakolu mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Wilaya, Sophia Masati.

Mteta alidai katika mashtaka hayo kuwa Novemba 15, katika ofisi za TRA, mshtakiwa alitoa fedha hizo za kigeni kumshawishi meneja wa TRA ampitishie maombi ya msamaha wa kodi.

Kodi hiyo ni malimbikizo ya kipindi cha kati ya mwaka 2013 na Oktoba 25, 2018.

Mtuhumiwa huyo anayetetewa na mawakili wawili, David Shilatu na Joseph Peter, alikanusha mashtaka hayo na mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kuweka masharti magumu ya dhamana kwa vile si raia.

Katika masharti ya dhamana, Hakimu Masati alimtaka mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh10 milioni, kusalimisha hati yake ya kusafiria na kutosafiri kwenda nje ya nchi.

Hadi saa 7:00 mchana jana, mshtakiwa alikuwa hajatimiza masharti ya dhamana. Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa uchunguzi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo kuahirishwa hadi Novemba 30.

Awali, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, mkuu wa Takukuru wa mkoa, Holle Makungu alidai mtuhumiwa huyo alikamatwa wakati akitoa fedha hizo kwa Mbibo.

Makungu alidai uchunguzi wao unaonyesha kuwa hadi Agosti 21, 2018, kampuni hizo mbili zilikuwa zikidaiwa malimbikizo ya kodi ya zaidi ya Sh5.7 bilioni, na kufikia Oktoba 25 ilikafikia Sh6.6 bilioni.

Alidai katika kushughulikia madeni hayo na kupata msamaha wa kodi, alionana na meneja huyo wa TRA mkoani Kilimanjaro na kuahidi kutoa kiasi hicho ili amsaidie kufanikisha maombi yake.

Baada ya kujiridhisha na uchunguzi wa awali, Makungu alidai mtego uliandaliwa na kufanikisha kumkamata Kakolu.

Wakati huohuo; Mahakama ya wilaya ya Iringa imemuachia kwa dhamana Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe aliyekamatwa jana akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa mzabuni wa ukusanyaji ushuru mkoani humo.

Akisoma mashtaka mawili yanayomkabili mtuhumiwa, Mwanasheria wa Takukuru, Restuta Kessy, alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Iringa, Liad Chamshama kuwa mshtakiwa anashtakiwa kwa makosa mawili.

Alidai kosa la kwanza ni la kushawishi kupokea rushwa ya Sh10milioni na kosa la pili ni kujipatia fedha kiasi Sh1.9 milioni kinyume na sheria.

Aliiambia Mahakama kuwa November 15 jioni akiwa katika Hoteli ya Gentle Hills mjini Iringa, Kimbe alikamatwa na Takukuru akiwa amepokea rushwa ya Sh1.9 milioni kutoka kwa Nancy Nyalusi ikiwa ni zawadi kutokana na kazi anazozifanya Nancy ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya kukusanya ushuru.

Mshtakiwa alikana kosa na Mahakama ilimuachia huru baada ya mtuhumiwa huyo kuweka bondi ya Sh10 milioni.

Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 15.

Chanzo: mwananchi.co.tz