Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atuhumiwa kukutwa na sare za JWTZ, kuwatapeli vijana

64769 Pic+mwanajeshi

Fri, 28 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Abubakari Makarabure (20) mkazi wa Kihonda manispaa ya Morogoro baada ya kukutwa akiwa amevaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa lengo la kuwatapeli vijana wanaotaka kujiunga na jeshi hilo.

Akizungumzia tukio hilo leo Ijumaa Juni 28, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbrod Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 15, 2019 maeneo ya Chawino akiwa na sare hizo na kujitambulisha yeye ni ofisa wa jeshi na ana uwezo wa kuwapatia vijana nafasi za kujiunga na jeshi ili baadaye wapate ajira.

Kamanda Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kumtapeli kijana aliyefahamika kwa jina la Hemedi Juma na wenzake wanne baada ya kumpa jumla ya Sh2.7 milioni ambazo alidai apewe kwa ajili ya fomu, vifaa pamoja na sare za mazoezi na gharama za kulipia kwenye kambi ya jeshi Lugalo, Dar es Salaam na Bulombora Kigoma ambako mafunzo hayo yataendeshwa.

 Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa alikiri kufanya utapeli huo hata hivyo polisi bado wanaendelea na uchunguzi kubaini mahali alikopata sare hizo kisha atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi huo kukamilika.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mutafungwa amewataka vijana wanaotaka kujiunga na jeshi kufuata utaratibu uliotangazwa na jeshi ili kuepuka kutapeliwa.

Katika tukio jingine, askari wa kampuni ya ulinzi ya Wigo, Mugisha Beyanga na mwenzake Johanes Jionas wanashikiliwa kwa tuhuma za kutoboa ukuta na kuiba mota nane za kiwanda cha kukobolea mpunga na kukamua alizeti zenye thamani ya Sh9.2 milioni.

Pia Soma

Mutafungwa amesema watuhumiwa hao walifanya wizi huo Juni 15, 2019 usiku ambapo baada ya kupekuliwa nyumbani kwake mlinzi huyo alikutwa na mota hizo.

 Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Chanzo: mwananchi.co.tz