Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu ashikiliwa mahabusu miezi minane, mawakili wachuana mahakamani

70186 Askofu+pic

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sakata la Askofu Mulilege Myondi Kameka anayeshikiliwa mahabusu kwa takribani miezi minane sasa kwa tuhuma za kutokuwa raia, limechukua sura mpya baada ya kuiomba Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, iwahukumu kifungo Kamishna wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kameka ambaye ni askofu wa Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship Church, lililoko Boko Magengeni, Dar es Salaam amefungua maombi hayo dhidi ya maofisa hao wa Serikali ya Tanzania, kwa kuendelea kumshikilia mahabusu licha ya mahakama hiyo kuamuru aachiwe huru kwa kupuuza amri yake.

Maombi hayo yaliyofunguliwa Julai 16, 2019, yalipangwa kusikilizwa leo Jumanne, Agosti 6, 2019 na Jaji Atuganile Ngwala lakini wajibu maombi waliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo.

Hivyo Mahakama hiyo imelazimika kusimamisha usikilizwaji wa maombi hayo na kusikiliza kwanza pingamizi hilo la awali, kama ilivyo kawaida ya taratibu za Mahakama.

Katika pingamizi lao la awali, wajibu maombi wamewasilisha hoja moja tu wakidai Mahakama hiyo haiwezi kuyasikiliza maombi hayo kwa kuwa haijaelekezwa sawasawa na mwombaji kwa kuwa kifungu cha sheria alichokitumia katika kufungua maombi hayo si sahihi.

Hata hivyo, wakili wa askofu huyo, John Mallya alipinga hoja za pingamizi hilo akidai  hazikidhi kuwa pingamizi la awali kwa kuwa pingamizi la awali linahusu hoja za kisheria tu lakini mawakili wa wajibu maombi katika hoja zao wameweka na maoni yao.

Pia Soma

Wakili wa Serikali ya Tanzania, Tuli Helela na Jackline Nyantori kwa nyakati tofauti waliieleza Mahakama kwamba kiutaratibu katika mazingira ya tuhuma za kosa wanalotuhumiwa wajibu maombi, mwombaji alipaswa kwanza kuwasilisha malalamiko yake polisi ndipo shauri lifunguliwe katika utaratibu wa hati ya mashtaka.

Walisisitiza katika utaratibu huo unatoa nafasi ya kuwaita mashahidi ili mlalamikaji athibitishe tuhuma zake bila kuacha mashaka yoyote, kisha Mahakama inapata nafasi ya kuchambua na kisha kutoa uamuzi.

Wakili Nyantori ameongeza hata kama Mahakama ikiamua kuyasikiliza maombi hayo kwa mtizamo wa jinsi mwombaji alivyoyawasilisha basi kosa hilo linalotuhumiwa si miongoni mwa makossa ambayo yanashtakiwa na Mahakama bali katika mahakama za chini.

“Kwa hiyo tunasema kwamba taratibu sahihi hazikufuatwa, hivyo tunaomba mahakama yako tukufu iyatupilie mbali maombi haya yote kwa kuwa haijaelekezwa vema,” amesisitiza Wakili Nyantori.

Wakili Mallya akijibu hoja hoza ameiomba Mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo la awali akidai halina vigezo vya kisheria kuwa pingamizi na kwamba madai ya mwombaji kwenda kuwasilisha malalamiko yake si utaratibu sahihi katika suala kama hilo.

Amedai kifungu cha 392 CPA kinataka kuwasilisha maombi kwa njia ya hati ya maombi na kiapo jambo ambalo ndilo walilofanya na kwamba kuhusu ushahidi wa kuthibitisha kosa hilo uko kwenye kiapo alichokiapa yeye kwa niaba ya mteja wake.

Wakili Mallya amedai kutokana na kuwepo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwa mmoja wajibu maombi basi Mahakama Kuu ndiko mahali sahihi pa kufungua maombi hayo kwa kosa hilo.

Jaji Ngwala amepanga kutoa uamuzi wake keshokutwa Alhamisi Agosti 8,2019 kuhusiana na pingamizi hilo la awali la wajibu maombi, ambao ndio utakaoamua kuendelea au kutokuendelea na maombi ya msingi ya kuwafunga maafisa hao.

Kwa mujibu wa amri ya kumshikilia na kumrejesha kwao askofu huyo iliyosainiwa Desemba 29, 2018 na Waziri wa Mambo ya Ndani, askofu huyo ni mhamiaji haramu ambaye yuko nchini kinyume cha Sheria.

Jaji Ilvin Mugeta, aliamuru aachiwe huru pamoja na mambo mengine kutokana na Serikali kutokujua asili ya uraia wake kuwa ni wa nchi gani hadi hapo itakapothibitika mahakamani kuwa si raia. 

Hata hivyo, licha ya uamuzi na amri hiyo ya Mahakama tangu Machi, 2019 ilipotolewa, bado askofu huyo anashikiliwa mahabusu katika gereza la Segerea.

Chanzo: mwananchi.co.tz