Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu ahojiwa Dar akituhumiwa utapeli

10175 ASKOFU+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam wanamhoji Askofu wa Kanisa la Agape Sactuary International, Martin Gwila kwa tuhuma za kuwatapeli watu mbalimbali wakiwamo maaskofu wenzake na taasisi mamilioni ya fedha.

Kuhojiwa kwa Askofu Gwila kunakuja wiki mbili baada ya Mwananchi, Julai 22 kuandika habari iliyofichua jinsi alivyowatapeli baadhi ya viongozi wa umma, makandarasi na taasisi kadhaa kwa kutumia kanisa lake.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boazi alilithibitisha gazeti hili, wiki hii kushikiliwa kwa askofu huyo aliyehojiwa Jumatatu katika ofisi za upelelezi (CID) Kamata jijini Dar es Salaam. Kwa sasa yuko nje kwa dhamana.

“Ni kweli tunafanya uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi ya mchungaji huyo. Wakati mwafaka ukifika tutatoa details (taarifa zaidi) za uchunguzi,” DCI Boaz aliliambia Mwananchi, juzi.

Habari zinasema makandarasi zaidi ya 20 na watu mbalimbali wamefungua polisi jalada la malalamiko ya kutapeliwa fedha na mchungaji huyo baada ya kuwasainisha mikataba ya kujenga makanisa katika maeneo mbalimbali nchini.

Inaelezwa pia kuwa polisi wanamchunguza kwa madai ya kuwatapeli watu fedha kwa ahadi ya kuwapatia kazi ikiwamo ya ulinzi katika taasisi yake.

Polisi wamethibitisha pia kuwa Gwila amehojiwa pamoja na Enock Samwel Raphael, anayedaiwa kuwa mtumishi katika halmashauri moja mkoani Arusha ambaye ni mshirika wa karibu wa askofu huyo.

Alipotafutwa kwa simu, Enock alikana kuhusiana karibu na Gwila, akidai alikwenda polisi kuwasilisha malalamiko ya kutapeliwa na askofu huyo.

“Hatuhusiani chochote, mimi nasali Lutheran na yeye ana kanisa lake. Mimi ni mkandarasi na sikuhojiwa ila nilikwenda polisi kupeleka madai yangu ya kutapeliwa na huyo Gwila.

“Alitapeli watu wengi na kampuni yangu na mimi ni mmojawapo. Kampuni yangu ilikuwa inajenga kanisa lake eneo la Duka Bovu, Arusha,” alisema Enock. Hata hivyo, nyaraka mbalimbazi za kanisa hilo ambazo Mwananchi linazo zinaonyesha kusainiwa na Enock ambaye alifanya kazi kama meneja na mshauri mkuu wa mradi wa Askofu Gwila wa kujenga makanisa 100 nchini.

Mtumishi huyo ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa mradi na amesaini baadhi ya nyaraka zilitotumwa na Gwila kwenda kwa makandarasi.

Alipoulizwa ni kwa nini jina na sahihi yake vimetumika katika barua kadhaa alizoziandika kwa niaba ya Askofu Gwila, Enock alikataa katakata kujadili suala.

Mwingine aliyehojiwa ni mtu aliyefahamika kwa jina moja la Suzan aliyewahi kufanya kama msaidizi wa karibu wa askofu huyo.

Akizungumza kwa masikitiko, mmoja wa makandarasi wanaodai kutapeliwa na askofu huyo, Julius Lucas ameliambia gazeti hili kuwa alitekeleza miradi miwili yenye thamani ya Sh284 milioni kila mmoja lakini hadi sasa hajalipwa.

“Kampuni yangu imeingia madeni makubwa. Pesa nyingine tulikopa na tumeshindwa kulipa kodi za Serikali. Ametuingiza kwenye hasara isiyoelezeka. Tunaomba vyombo vya dola vimchunguze ili tuweze kurejeshewa pesa zetu,” alisema Lucas ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya ukandarasi ya Lucas Construction.

Tayari Askofu Gwila amehojiwa na polisi mkoani Dodoma kwa madai ya utapeli.

Hivi karibuni kamanda wa polisi mkoani humo Gilles Muroto aliwaambia waandishi huku akiwa na askofu huyo kuwa anatuhumiwa kuwatapeli watu mbalimbali na kujipatia zaidi ya Sh68 milioni kwa ahadi ya kuwaajiri.

Pia anadaiwa kuwatapeli viongozi mbalimbali wa Serikalini na wastaafu pamoja na taasisi kwa ahadi ambazo zimelalamikiwa kuwa za uongo.

Juhudi za kumpata askofu huyo kwa siku kadhaa sasa hazijazaa matunda, ila zinaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz