Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari wanaodaiwa kuiba Sh90 milioni, wakosa dhamana

Askari Wezi Weziiii.png Askari wanaodaiwa kuiba Sh90 milioni, wakosa dhamana

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maofisa watatu wa Jeshi la Polisi nchini akiwemo mwanamke, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha na kujipatia Sh90 milioni, mali ya Grace Matage.

Askari hao ni mwenye namba F 7149 D/ Coplo Ramadhani(42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa, mwingine ni mwenye namba G. 7513 D/ Coplo Majid Abdallah(35) mkazi wa Kunduchi na askari wa kike mwenye namba WP 6582 D/ Coplo Stela Mashaka.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Oktoba 31, 2023 na kusomewa shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akiwasomea shtaka lao wakili wa Serikali, Neema Moshi amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai.

Wakili Moshi amedai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 katika eneo la Kurasini, karibu na ofisi za Uhamiaji.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.

Amedai kuwa washtakiwa hao kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili kujipatia fedha hizo bila kikwazo.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalowakabili walikana kutenda kosa hilo, huku upande wa mashtaka ukidai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa shauri hilo, na kuiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Msumi amewaambia washtakiwa hao kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kubaki rumande.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Ndugu na jamaa watoa machozi mahakamani

Baada ya Hakimu Msumi kuwaeleza washtakiwa hao kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, baadhi ya ndugu jamaa na marafiki waliofurika katika Mahakama ya wazi namba mbili, waliinamisha vichwa chini huku wengine machozi yakiwatiririrka na kutafuta na kitambaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live