Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari wa zamu asimulia anayodai kuyashuhudia kituoni usiku mnene

Mauaji Polisi Mtwara Askari wa zamu asimulia anayodai kuyashuhudia kituoni usiku mnene

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa tano katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Polisi mkoani Mtwara ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio hilo usiku washtakiwa wawili walifika kituoni cha Polisi Mitengo na kumbeba mtu kwenye machela wakaondoka naye.

Hata hivyo, alipohojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu, amekiri kuwa hakumfahamu mtu huyo kwa jina, mahali alikotolewa na alivyoingizwa kituoni hapo na wala hakujua kama alikuwa amefariki au alikuwa mgonjwa tu.

Shahidi, huyo Sajenti Jagati Samson, kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ameyaeleza hayo leo Novemba 21, 2023 katika kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inayosikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Mbuta Chigingozi, Mkaguzi wa Polisi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara, mkoani Mtwara, Januari 5, 2022.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, walifikia uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwake wakimtuhumu kuvunja na kuiba pikipiki na fedha hizo.

Askari asimulia

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ignas Mwinuka, Sajenti Jagati ameeleza kuwa siku hiyo ya tukio, Januari 5, 2022, aliingia zamu ya ulinzi kituoni hapo na askari wake watatu.

Amedai kuwa wakiwa wanaendelea na ulinzi, usiku wa saa 6 kuelekea saa 7 aliona gari katika barabara ya Mtwara - Lindi likitokea uelekeo wa Mtwara mjini na lilipofika usawa wa kituo hicho liliacha barabara hiyo na kifauta njia ya kuingia kituoni hapo.

Amesema lilipofika getini alilimulika kwa tochi akabaini ni gari la Polisi aina ya Land Cruiser, na alipolimulika lilisimama likazima taa za nje na kuwasha taa za ndani na akaliruhusi liingie kituoni taratibu.

Alilisogelea na kuwatambua waliokuwemo kuwa ni OCS wa kituo cha Mtwara mjini, ASP Onyango (mshtakiwa wa pili), aliyekaa mbele kushoto na dereva alikuwa OC-CID Mtwara mjini SP Kalanje (mshtakiwa wa kwanza).

Sajenti Jagati amedai kuwa nyuma pia kulikuwa na watu wawili ambao alimtambua mmoja ambaye alikuwa ni Mkaguzi msaidizi, Grayson lakini mwingine hakumtambua maana alivaa kofia ya kitambaa iliyofunika kichwa na uso wote na kuacha macho pekee.

Hivyo aliwakaribisha na ASP Onyango akasema kuwa wamekwenda kumchukua mgonjwa wao na akawataka wao waendelee na ulinzi.

"Waligeuza gari wakaisogeza usawa wa mlango wa chumba cha mashtaka kituoni ambapo Afande Kalanje na Afande Onyango wakashuka na kuingia ndani na kisha wale waliokaa nyuma nao wakashuka na machela.

"Nilishikwa na wasiwasi kwa kuwa funguo za zile mahabusu nilikuwa nazo na pili hatukuwa tumepewa taarifa kama kuna mtu atakuja kuchukuliwa hapa tofauti na watuhumiwa tunaowalinda. Hivyo nilijiuliza hao wana funguo gani za kwenda kufungulia huko?

Kutokana na wasiwasi huo, amesema aliamua kuwafuatilia, kwa nyuma ajue wanaelekea wapi, lakini hawakuelekea mahabusu bali walikwenda kwenye chumba kinachotumika kama stoo huku yeye akiwachungulia kwa kuibiaibia aliwaona wote wakaingia kwenye chumba hicho.

Amedai kuwa walipoingia humo walirudishia mlango na hakuona tena kilichoendelea, lakini akaendelea kusubiri mpaka watakapotoka na kwamba baada ya dakika kama 15 walitoka wakiwa wamebeba mtu kwenye machela hiyo.

Sajenti Jagati amedai kuwa mtu huyo alibebwa na Grayson na yule mtu mwingine wakiwa wametangulia na SP Kalanje na ASP Onyango wakifuata kwa nyuma.

"Huyo mtu alikuwa mtu mzima alikuwa amelala chali na akiwa hatikisiki na walimuingiza harakaharaka kwenye gari na ASP Onyango akatutaka tuendelee na kazi.

"Walivyotoka pale walielekea Mtwara mjini lakini baada ya muda kama wa dakika 10 gari hilo likapita tena Iikitokea Mtwara mjini kuelekea uelekeo wa Lindi.

Alidai kuwa alimjulisha mkuu wake wa kikosi kuhusu taarifa hizo ambaye alisema kama kuna lolote watajua.

Amesema kuwa Januari 21, 2022 aliitwa kwa RCO ambavye alimtaka aeleze kuwa anajua nini kilichotokea katika kituo hicho Januari 5, 2022 naye akaeleza kile alichokishuhudia kwa macho yake na RCO akamuagiza akaandike maelezo yake na askari aitwaye Mwimba.

Maswali ya dodoso

Baada ya maelezo hayo shahidi huyo aliohojiwa maswali ya dodoso na Wakili Magafu anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje na Wakili Fredrick Ododa, anayemtetea mshtakiwa wa pili, ASP Onyango. kama ifuatavyo

Wakili Magafu: Shahidi mpaka hapo uliposimama leo hii yule mtu aliyebebwa kwenye machela unamfahamu?

Shahidi: Hapana

Wakili: Hujui jina lake wala wapi alikotokea mpaka kufika pale?

Shahidi: Hapana simjui

Wakili: Na mpaka sasa hujui kama alikuwa marehemu au alikuwa mgonjwa tu?

Shahidi: Mimi sijui kama alikuwa marehemu, niliona amelala tu.

Wakili: Huyu Afande Onyango na Afande Kalanje unajua hizo funguo walitoa wapi?

Shahidi: Sijui maana hawakugusa eneo langu la ulinzi.

Wakili: Uliwahi kumuuliza Koplo Ahmad (aliyemkabidhi zamu) kuwa hao maofisa walipata wapi funguo za hicho chumba?

Shahidi: Sikuwahi kumuuliza.

Wakili: Lakini kitendo cha hawa kuingia kule ndani na kufungua kile chumba na funguo za mahabusu unazo wewe ndio kilikutia wasiwasi?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Kama kile kitendo kilikutia wasiwasi kwa nini hukumuuliza Ahmad funguo walipata wapi?

Shahidi: Sikumuuliza kwa sababu sehemu waliyofungua mimi hainihusu.

Wakili: Nani alikupa taarifa kuitwa na RCO (Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai wa Mkoa)?

Shahidi: Nilipewa na kiongozi wangu wa kikosi, Meja Frank.

Wakili: Kwani haikuwa kawaida hawa viongozi kutembelea kile kituo?

Shahidi: Ni kawaida maana pale tunakaguliwa na viongozi.

Wakili: Unamfahamu aliyekuwa mkuu wa kituo cha pale Mitengo?

Shahidi: Ndio, anaitwa Afande Kiula.

Wakili: Uliwahi kumpa hiyo taarifa Kiula?

Shahidi: Hapana sikuwahi kumpa hiyo taarifa.

Wakili: Kwa hiyo mpaka leo hii hujawahi kuongea naye hiyo taarifa?

Shahidi: Sijawahi kuongea naye.

Wakili: Umesema walikuja na Land Cruiser ya Polisi unaijua namba zake?

Shahidi: Hapana sikuzijua.

Wakili: Unakubaliana na mimi kuwa Land Cruiser za Polisi nyingi zinafanana kwa mwonekano?

Shahidi: Hapana, sikubaliani na wewe kwamba zinafanana.

Wakili: Ni kitu gani kinachozitofautisha?

Shahidi: Zinatofautiana kwa ukubwa, namba na kwa rangi.

Wakili: Hii waliyokuja nayo ilikuwa na kitu gani kinachozitofautisha na nyingine?

Shahidi: Niliitambua kwa rangi na ukubwa.

Shahidi: Utakubaliana na mimi kwamba gari hutofautishwa kwa namba zake hata zikiwa za aina moja?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Siku hiyo Afande Onyango alivaa nguo za aina gani?

Shahidi: Sikumbuki

Wakili:. Afande Kalanje alivaa nguo gani?

Shahidi: Sikumbuki

Wakili: Na Grayson unajua aliko?

Shahidi: Sifahamu, najua amefariki

Wakili: Na yule aliyejifunika uso hujawahi kumjua?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Na wala yule mtu hujui alifikishwa pale muda gani na lini?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili Ododa: Shahidi ni sahihi au si sahihi kwamba hujatoa nyaraka yoyote hapa mahakamani kuonyesha Januari 5, 2022 ulikuwa katika kituo chako cha kazi Mitengo?

Shahidi: Hauko sahihi

Wakili: Nitakuwa sahihi pale Mitengo kuna kitu kinaitwa duty roster (mpango kazi), kitabu cha kumbukumbu kwa askari wanaoingia zamu na kutoka?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba kitabu hicho cha kumbukumbu cha Januari 5, 2022 kuonyesha kuwa uliingia kazini siku hiyo hakipo hapa mahakamani?

Shahidi: Hauko sahihi.

Wakili: Ni kweli au si kweli kwamba Januari 5, 2022 ulisaini kitabu hicho kuonyesha kwamba umeingia kazini tarehe hiyo?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Kutokuwepo kwa hicho kitabu hapa maana yake hakuna ushahidi kwamba ulisaini na kuingia kazini siku hiyo, nitakuwa sahihi?

Shahidi: Hauko sahihi.

Wakili: Ni kweli kwamba chumba hicho (walimoingia kina Kalanje) ni sehemu yako ya ulinzi?

Shahidi: Ni kweli.

Maswali ya ufafanuzi kutoka kwa wakili wa Serikali, Mwinuka

Wakili wa Serikali: Shahidi uliulizwa na wakili Magafu kuhusiana na kutompa taarifa mkuu wa kituo cha Mitengo ukasema hukumpa taarifa kwa sababu, lakini akakukatisha sasa hebu elezea ni kwa sababu gani hukumpa taarifa?

Shahidi: Sikumpa taarifa kwa sababu wakati tunakabidhiana yeye hakuwepo.

Kwa upande wake wa shahidi wa sita Sajenti Mwaya Salimin Mwaya ambaye ni mtunza vielelezo katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara ameieleza Mahakama kuwa aliwaona washtakiwa hao wawili na Grayson wakiondoka kituoni hapo wakiwa na machela.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Kassim Nassri amedai kuwa siku ya tukio Januari 5, 2022 alikuwa zamu ya usiku akiwa msimamizi wa chumba cha mashtaka (CRO).

Amedai kuwa saa 5:00 usiku alifika SP Kalanje, akaenda ofisini kwake ghorofani na baadaye kidogo alifika ASP Onyango akaingia ofisini kwake na baada ya muda kidogo alifika Mkaguzi msaidizi Grayson akapanda juu ghorofani.

Shahidi huyo ameeleza kuwa baada ya dakika kama 15 aliteremka SP Kalanje akampitia ASP Onyango wakatoka nje wakaenda mbele ya kituo cha kwenye maegesho ya magari.

"Baadaye kidogo Mkaguzi msaidizi Grayson alitokea nyuma ya kituo akapita CRO akiwa amebeba machela akaelekea kwa kina SP Kalanje na ASP Onyango waliokuwa kwenye magari", alieleza Sajenti Mwaya na kuongeza:

"Grayson aliingia kwenye gari ya Polisi namba PT1918 upande wa nyuma pamoja na ile machela. OCS Onyango naye aliingia akakaa mbele pembeni mwa dereva na OC-CID Kalanje akaendesha hilo gari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live