Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari wa Tawa kortini wakidaiwa kuua watu sita

HUKUMU Askari wa Tawa kortini wakidaiwa kuua watu sita

Fri, 1 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tabora. Askari sita wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wamefikishwa Mahakama kuu Kanda ya Tabora, wakishtakiwa kuua watu sita katika hifadhi ya Ugalla iliyopo wilayani Sikonge.

Mahakama hiyo imeanza kusikiliza shauri hilo la Jinai namba 111 la mwaka 2023 Novemba 29, mwaka huu baada ya askari hao kudaiwa kufanya tukio hilo wakati wakifanya doria ndani ya hifadhi hiyo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda mauaji hayo Julai 27, 2022 kinyume na kifungu cha 196 na 197 sura ya 16 ya kanuni ya adhabu ambao wamekana kuhusika na mauaji hayo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Zainab Mango.

Askari wanaoshtakiwa ni Shoka Haruna, David Kalikumbi, Mussa Nyarukende, Rosta Muigi, Ally Mussa na Abbas Mgweno wote kwa pamoja wakidaiwa kufanya mauaji ya Salum Said, Rajab Julius, Lule Mhidi, Baraka Dotto, Ally Said na Jackson Said.

Mahakama hiyo imesikiliza ushahidi wa shahidi wa kwanza kati ya mashahidi 26 ambaye ni Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Sikonge, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Kisu Mwapongo aliyeieleza namna washitakiwa hao walivyokwenda kuonesha miili ya marehemu walipoitelekeza ndani ya hifadhi ya Ugalla.

Ameeleza kuwa mahali walipooneshwa miili ya watu hao, walikuta maganda ya risasi za silaha aina ya SMG au AK 47 zilizokuwa zikitumiwa na washtakiwa hao katika doria waliyokuwa wakifanya.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mawakili wanne wakiongozwa na Wakili Merito Ukongoji ambao walimpeleka shahidi wa kwanza kuwasilisha ushahidi wake ambaye aliieleza Mahakama kwamba amewatambua washtakiwa wote sita waliokuwepo mahakamani ndio waliowakamata kwa kuhusika na tuhuma za mauaji hayo.

Shauri hilo linaendelea leo Novemba 30, 2023 ambapo upande wa Jamhuri utamuita shahidi wake wa pili kati 26 kutoa ushahidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live