Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari polisi mstaafu atuhumiwa kujeruhi kwa kitu kizito

50349 Pic+askari

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imeelezwa jinsi mgogoro wa mipaka ulivyopelekea askari mstaafu wa Jeshi la Polisi, Fortunatus Nyigana (66) kumjeruhi kwa  kitu kizito jirani yake Hashimu Msekwa (61).

Hayo yameelezwa leo mbele ya Hakimu Mkazi, Adolf Schore na wakili wa Serikali, Teddy Mtao na mlalamikaji katika kesi hiyo Msekwa wakati akitoa ushahidi wake.

Msekwa alidai yeye na Nyigana hawana ugomvi wowote ila aliwahi kutoa ushahidi wa mipaka kwa jirani yake aliyenunua nyumba iliyokuwa inamilikiwa na dada yake dhidi ya Nyigana kwa sababu wakati wanaoneshana mipaka  yeye alikuwapo.

Alieleza wanaishi Tabata Mtambani na kwamba Agosti 19, 2018 nyakati za jioni akiwa nyumbani kwake na mafundi  nane wakijadiliana kujenga shimo walilolichimba ghafla alitokea Nyigana kwa nyuma yao.

Alidai Nyigana alimueleza alikuwa akimtafuta kwa kutoa ushahidi wa uongo na kumtisha kuwa siku hiyo ndiyo utakuwa mwisho wake.

Akiendelea kutoa ushahidi, Msekwa alidai Nyigana alikuwa ameshika mkononi Ila hakuweza kujua ni cha aina gani na kumpiga nacho kichwani akaanguka na kupoteza fahamu.

Alidai wenzake alikuwa nao walimchukua wakampeleka polisi kupata PF3 na baadaye hospitali ambapo alipatiwa matibabu na kushonwa nyuzi 12 kichwani.

Aliendelea kudai kuwa polisi walifika kujua chanzo cha tukio hilo na kwamba kinahusiana na yeye kutoa ushahidi wa kiwanja kilichouzwa na dada yake kwa sababu anakifahamu dhidi ya Nyigana.

Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, Hakimu Sachore aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23 ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Kwa mujibu wa kesi hiyo ya jinai namba 527,2018, Nyigana anadaiwa kuwa Agosti 19, 2019 huko Tabata Mtambani alimpiga Msekwa kwa kitu kizito kichwani na kumsababishia majeraha.



Chanzo: mwananchi.co.tz