Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari feki wa JWTZ akamatwa Morogoro

50085 Askaripic

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limemkamata mtu mmoja anayedaiwa kuwa askari feki wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Fadhil Yahaya (29) alikutwa na sare zinazofanana na za jeshi hilo kwenye kituo cha mabasi Msamvu akiwa na vyeo vya kapteni

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa askari feki huyo ambaye ni mkazi wa Kigamboni alikuwa akiendesha gari dogo aina ya Vitz nyeusi ambapo pea moja ya sare hizo aliining’iniza juu ya siti ya gari.

Kamanda Mutafungwa amesema kuwa askari feki huyo alikamatwa na polisi waliokuwa doria katika eneo hilo baada ya kupewa taarifa na wasamaria wema ambao walimtilia mashaka na baada ya kumpekua walikuta sare pamoja na vyeo vya jeshi hilo.

Amesema kuwa katika uchunguzi uliofanywa na polisi wamebaini kuwa mtuhumiwa huyo ni mzoefu na alishawahi kuhusika katika matukio mbalimbali ya utapeli kwa kutumia sare hizo na tayari alishafikishwa mahakamani kwa makosa hayo.

Kamanda Mutafungwa amesema kuwa Machi 26, 2014 huko Mahenge wilaya ya Ulanga mtuhumiwa huyo alitapeli Sh350,000 kutoka kwa vijana mbalimbali akiwaahidi kuwatafutia nafasi za kujiunga JWTZ na tayari kesi ya jinai namba 164 imeshafunguliwa katika mahakama ya wilaya ya Ulanga.

Amesema kuwa Oktoba 21 mwaka jana mtuhumiwa huyo pia alikwenda ofisini kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Ulanga na kujitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ mwenye cheo cha Luteni Ussu lakini alitiliwa mashaka na baada ya kupekuliwa alikutwa na vyeo mbalimbali vya JWTZ pamoja na sare za jeshi hilo.

Kufuatia tukio hilo Kamanda Mutafungwa amesema uchunguzi zaidi unaendelea kwa kushirikiana na JWTZ ili kubaidi uhalali wa sare hizo na namna mtuhumiwa alivyozipata ama kutengeneza na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi huo kukamilika.



Chanzo: mwananchi.co.tz