Baadhi ya askari wa polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/Rorya wanadaiwa kuwa kikwazo katika mapambano dhidi ya ukeketaji kwa kuwalinda watuhumiwa kutokana na ushawishi wa rushwa.
Tuhuma hizo zimeibuliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju aliyetahadharisha kwamba siku za askari hao aliodai tayari wizara ina majina ya zinahesabika.
“Haiwezekani Serikali imetumia fedha nyingi kuanzisha Kanda Maalum ya Polisi Tarime/Rorya kudhibiti uhalifu halafu baadhi ya askari polisi wakwamishe juhudi za kukomesha ukeketaji kwa kuwataarifu watuhumiwa operesheni za kuwakamata zinapoandaliwa. Siku za askari hao zinahesabika kwa sababu tayari tunayo majina yao,” alisema Mpanju alipofunga kilele cha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji.
Ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania uliofanywa mwaka 2015/16 inaonyesha Mara ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji nchini ikiwa na asilimia 32. Mikoa mingine ni Manyara (58), Dodoma (47), Arusha (41) na Singida wenye asilimia 31.
Akizungumzia hali ya ukeketaji eneo la Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, mkuu wa dawati la jinsia wa kanda hiyo, Cloud Mtweve alisema matukio 15 yaliripotiwa ndani ya miaka miwili iliyopita zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa watuhumiwa 19.
“Matukio matano yalifikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika lakini mawili yalimalizika kwa washtakiwa kuhukumiwa adhabu tofauti huku mashauri matatu yapo katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali,” alisema Mtweve.
Alisema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa 41 za majaribio ya ukeketaji ambayo yalizuiwa hivyo kuwaokoa wasichana waliokuwa wakeketwe.
“Zaidi ya watoto 400 waliokuwa hatarini kukeketwa waliokolewa kwa juhudi za dawati la jinsia na wadau wengine wanaoshiriki vita dhidi ya ukeketaji. Watoto hao walipelekwa kuhifadhiwa katika vituo vya nyumba salama katika wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama,” alisema Mtweve.
Akizungumzia changamoto zinazokwamisha vita hivyo, Mtweve alisema ukeketaji unajumuisha familia kutoka Tanzania na Kenya hivyo ukidhibitiwa upande mmoja wanahamia mwingine.
“Ukeketaji ni organized crime (uhalifu wa kimtandao) kati ya wanajamii inayopatikana katika nchi zetu mbili. Tunapofanya msako na operesheni upande wetu watuhumiwa wanahamia upande wa pili vivyo hivyo operehseni ikifanyika upande ule, wanahamia huku kwetu kutokana na mwingiliano wa kijamii katika maeneo haya,” alisema.
Changamoto nyingine alisema baadhi ya ndugu, marafiki na majirani wenye taarifa muhimu hawaendi polisi kuandikisha maelezo au mahakamani kutoa ushahidi hivyo washtakiwa kuachiwa huru.
“Ukeketaji ni kosa kisheria bila ushahidi usioacha shaka lolote ni vigumu washtakiwa kutiwa hatiani na kuadhibiwa kwa matendo yao. Kuna wakati hata watoto wanaofanyiwa vitendo huwa wagumu kutoa ushahidi dhidi ya wazazi wao,” alisema Mtweve.
Katika kukabiliana na changamoto ya watuhumiwa kuvuka mpaka, alisema viongozi wa Serikali katika wilaya na mikoa inayopakana kati ya Tanzania na Kenya wameunda kikosi kazi.
“Wenyeviti wa kamati ni mkuu wa Wilaya ya Tarime na mwenzake wa Wilaya ya Kurya upande wa Kenya. Kwa juhudi hizi za pamoja tunaamini tutafanikiwa kukomesha ukeketaji,” alisema Mtweve.
Mchungaji wa Kanisa la EAGT la mjini Tarime, Jakson Nyaburiri alisem akuna umuhimu wa jamii kubadilika kwa kutoa taarifa zitakazosaidia washiriki wa ukeketaji kutiwa mbaroni kisha kutoa ushahidi mahakamani waadhibiwe kisheria.
Umuhimu wa jamii kubadilika pia ulisisitizwa na Askofu wa Kanisa la Nazareth mjini Tarime, Thobias Oluoch aliyeiomba Serikali kuongeza ushirikiano kukomesha ukatili huo ndani ya jamii.
Aliyekeketwa, ngariba wafunguka
Wankyo Wambura, mmoja wa washiriki wa kongamano hilo aliyekiri kuwa miongoni mwa wanawake waliokeketwa aliiomba Serikali kukomesha mauaji ya vikongwe na wenye ualbino pamoja na ukeketaji.
“Mimi ni mwathirika wa ukeketaji, sina furaha kwenye ndoa yangu kutokana na maumivu nayoyapata wakati wa kushiriki tendo la ndoa. Miaka ya nyuma kibofu cha mkojo kilipasuka wakati najifungua. Naoimba Serikali ikomeshe vitendo hivi kuwanusuru watoto na wajukuu wetu,” alisema Wankyo.
Nchagwa Warioba, mwanaume aliyeoa mwanamke aliyekeketwa alisema ipo tofauti wakati wa tendo la ndoa kati ya mwanamke aliyekeketwa na asiyekeketwa.
“Binafsi sijawahi kufurahi kushiriki na mmoja wa wake zangu aliyekeketwa kutokana na anavyolalamika kuumia. Msiniulize huwa nafanyaje lakini huo ndio ukweli. Nawasihi ndugu zangu tuachane na mila hii,” alisema Nchagwa
Mmoja wa mangariba walioacha kazi hiyo baada ya kuelimishwa na kujua madhara ya ukeketaji, Bhoke Mbusiro aliisihi jamii kuachana na vitendo hivyo na kuitaka kuwalinda mangariba walioacha kazi na kujitangaza dhidi ya vitisho wanavyopata.
“Vitisho huzidi pindi mwanajamii anapokamatwa kwa sababu jamii inahisi sisi ndio tumetoa taarifa. Serikali itulinde,” alisema.
Madhara ya ukeketaji
Akizungumzia madhara ya ukeketaji, Dk Mahende Juma wa Kituo cha Afya cha Hope kilichopo Musoma Mjini alisema ni kutokwa damu nyingi wakati wa ukeketwaji na ule wa kujifungua.
“Baada ya kukeketwa mwanamke hupata kovu ambalo huchanika wakati wa kujifungua na kusababisha kupoteza damu nyingi. Hii inahatarisha afya ya mama na mtoto,” alisema Dk Mahende.
Ukeketaji pia alisema unawaweka wahusika kvirusi vya Ukimwi kutokana na kufanyika kwa usiri na njia isiyo salama kiafya.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alisemwa “mila nyingine tunatakiwa kuzipima kwani siyo kila tulichokirithi kinafaa. Ukeketaji una madhara makubwa ikiwamo maambukizi ya Ukimwi, kupoteza damu na vifo kwa watoto na wanawake waliokeketwa. Tubadilike.”