Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari Polisi akamatwa Manyara akiwa na madawa ya kulevya

Askari Polisi Akamatwa Manyara Akiwa Na Madawa Ya Kulevya Askari Polisi akamatwa Manyara akiwa na madawa ya kulevya

Wed, 19 Jul 2023 Chanzo: Ngilisho

Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linawashikilia askari Polisi wawili, akiwemo Mrakibu Msaidizi wa Kituo cha Polisi Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, John Shauri na raia mmoja kwa kosa la kusafirisha shehena ya dawa za kulevya aina ya Mirungi gunia nne yenye bunda kilao 264.

Askari Polisi Shauri, alikamatiwa jiji Arusha baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi katika kizuizi cha ukaguzi cha Minjingu Mkoani Manyara Julai 14, mwaka huu.

Kukamatwa kwa Askari huyo kumethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Manyara, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Nchini (ACP), Lucas Mwakatundu na kusema kuwa askari huyo alikamatwa Julai 16 mwaka huu, jijini Arusha.

Kamanda Mwakatundu alisema kuwa baada ya kukamatwa alipelekwa Makao Makuu ya Polisi Babati na kusweka rumande ili aweze kujibu shitaka linalomkabili ndani ya jeshi hilo kabla ya kupata maelekezo mengine kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo.

"Ni kweli askari Shauri anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma hizo na yuko rumande akisubiri taratibu za Kipolisi ndani ya Jeshi hilo kabla ya maelekezo mengine kutoka kwa viongozi wa Juu wa Jeshi hilo," alisema Mwakatundu.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Manyara zilisema kuwa askari Shauri aliyekuwa akiendesha gari aina ya Noah Vox rangi nyeusi yenye namba za usajili T465CUS ilikamatwa majira ya ya saa 2.30 asubuhi akiwa na shehena hiyo ya mirungi ikiwa imejaa kwenye gari hiyo.

Awali, askari huyo alisimamishwa na kikosi cha doria cha Polisi Babati na kikosi hicho kilikuwa kikiongozwa na operesheni ofisa wa Polisi Babati Mrakibu Msaidizi {jina tunalo} baada ya kupata taarifa fiche kutoka kwa raia wema juu kusafirisha mara kwa mara kwa mirungi hiyo kunakofanywa na askari huyo asiye na weledi kutoka Arusha kwenda Babati.

Vyanzo vya habari vya polisi Babati viliendelea kusema kuwa askari Shauri alikuwa akifanya biashara hiyo haramu ya kusafirisha Mirungi akiwa na sare za jeshi la polisi ili iwe njia rahisi yeye kupita katika vizuizi mbalimbali vya polisi Makuyuni, Minjingu na Babati.

Habari zaidi zilisema kuwa alipofika katika kizuizi cha Minjingu alisimamishwa na askari na aliposogelewa ili kufanyiwa ukaguzi aliondoa gari kwa kasi na kukimbia ndipo hatua ya kulikimbiza gari hilo ilipoamuriwa na Mkuu wa Operesheini Babati.

Vyanzo vya Kipolisi Babati vilisema kuwa baada ya kukimbizwa na kufikiwa kwa karibu ili aweze kuzuiwa na crusser ya polisi, Shauri alipaki gari pembeni na kulitelekeza gari hilo na kutokomea msituni kusikojulikana.

Vyanzo viliendelea kusema kuwa baada ya hatua hiyo ya askari Shauri kutokomea kusikojulikana, Mkuu wa Operesheni Babati akiwa na askari wengine kwa kushirikianana raia wema waliokwenda katika tukio hilo walipekua gari hiyo na kukuta sare kadhaa za Jeshi la Polisi, Kitambulisho cha Polisi, Kadi za Benki mbalimbali, vitambulisho vya NIDA, Tume ya Uchaguzi, Bima ya Afya na ikabainika kuwa askari huyo ni wa kituo cha Polisi Arumeru Mkoani Arusha.

Baada ya upekuzi huo kumalizika gari hiyo ilivutwa na break Down hadi Kituo Kikuu cha Polisi Babati na kukabidhiwa kwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Manyara kwa hatua zaidi.

Hata hivyo habari zaidi kutoka Polisi Babati na Arusha zilisema kuwa askari Shauri ambaye yuko katika mafunzo ya utimamu wa mwili katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani Arusha{FFU} chini ya Mrakibu Mwandamizi{CCP} Mikidadi Galilima ambaye ndiye msimamizi Mkuu wa Mafunzo hayo aliombwa ruhusa siku hiyo majira ya saa 11.30 alfajiri Julai 14 mwaka huu na askari huyo kuwa anaumwa na alipewa mapumziko siku hiyo bila kupewa hati ya matibabu{sick sheet}.

Vyanzo vilisema kuwa baada ya kupewa ruhusa hiyo ndipo safari ya kuanza kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Mirungi ilipoanza kutoa Arusha kwenda Babati.

Baadhi ya askari Polisi Mkoani Arusha na Manyara walisema kuwa kuendelea kwa matukio ya uhalifu kwa askari wakubwa wa jeshi hilo katika Mikoa hiyo ni kutokana na baadhi ya hatua stahiki kutochukuliwa kwa baadhi yao kwani kuna matukio mengine manne yamefanyika arusha hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Vyanzo kutoka ndani ya jeshi hilo Arusha na Manyara vilisema kuwa miongoni mwa matukiuo hayo ni pamoja na askari kukiri kupokea rushwa na kurudisha zaidi ya shilingi milioni 9 katika matukio ya Ngaramtoni na Kwa Mrombo kwani Vigogo wa polisi Arusha wamekuwa wakiwalinda vigogo wenzao.

Chanzo: Ngilisho