Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari Magereza adaiwa kumuua mfugaji kwa kumpiga risasi, baba agoma kuzika mwanae

49269 MAGEREZA+PIC

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Lepeli Mandero (20) ameuawa kwa kupigwa risasi na mtu anayedaiwa kuwa askari wa Jeshi la Magereza baada ya kuingiza mifugo kwenye shamba la gereza la Mbigiri lililopo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, huku baba wa marehemu, Tingu Kurumeti akigoma kufanyika mazishi ya mwanaye mpaka mwili ufanyiwe uchunguzi ili askari aliyefanya kitendo hicho achukuliwe hatua.

Tukio hilo lilitokea jana mchana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ambaye alisema alikuwa akielekea eneo la tukio ili aweze kutoa taarifa zaidi.

Akizungumzia tukio hilo baba wa marehemu, Kurumeti amesema hawezi kufanya mazishi ya mwanaye mpaka mwili ufanyiwe uchunguzi na askari aliyefanya kitendo hicho kuchukuliwa hatua.

Shuhuda wa tukio hilo, Sumaye Sadru amedai mbali na kufanya mauaji hayo, askari huyo pia aliwapiga risasi ng'ombe watano ambao nao walikufa na wengine zaidi ya 100 kuchukuliwa.

Amedai eneo la tukio halikuwa na mazao yoyote na kabla ya kufanya mauaji hayo askari huyo aliwakimbiza huku akipiga risasi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,  Dk Stephen Kebwe amezungumzia tukio hilo na kwamba askari watatu wa Magereza wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano juu ya tukio hilo.

Amewataka wafugaji kuwa wavumilivu wakati huu ambako uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.



Chanzo: mwananchi.co.tz