Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asakwa na polisi kwa kujeruhi mume kwa kisu

102226 Pic+kisu Asakwa na polisi kwa kujeruhi mume kwa kisu

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Jeshi la polisi mkoani Shinyanga linamsaka Suzana Richard mkazi wa Uzogole Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumjeruhi mume wake kwa kuchoma kisu ubavuni baada ya kutokea kutoelewana kati yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumchoma kisu mumewe Mpemba Gamba (48) katika tukio lililotokea saa 6:00 usiku wa Aprili 11, 2020 wakiwa nyumbani kwao mtaa wa Uzogole Manispaa ya Shinyanga.

Kabla ya tukio hilo, wanandoa hao wanadaiwa kuwa na mvutano kuhusu kurudiana baada ya kutengana siku tatu zilizopita.

"Mtuhumiwa alikimbia na kutokomea kusikojulikana. Polisi tunaendelea kumsaka ili kumfikisha mahakamani  kujibu tuhuma dhidi yake," amesema Kamanda Magiligimba

Akifafanua, Kamanda Magiligimba amesema  mtuhumiwa na mume wake walitenga siku tatu kabla ya tukio na siku hiyo alirejea nyumbani kumshawishi mume wake warudiane na baada ya ombi lake kukataliwa ndipo alimjeruhi mwenzake kwa kumchoma kisu ubavuni.

"Tunawasisitiza wanandoa na watu walioko kwenye  mahusiano ya mapenzi kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapotofautina  badala yake watafute msaada wa kisheria au ushauri wa wazazi, wazee na viongozi wa kijamii na kidini," ameshauri Kamanda  Magiligimba.

Chanzo: mwananchi.co.tz