Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayetuhumiwa kumuua mkewe, kumchoma moto ataka kuonana na hakimu

Mstakiwa Pic Anayetuhumiwa kumuua mkewe, kumchoma moto ataka kuonana na hakimu

Thu, 29 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mshtakiwa Hamis Luongo (41) maarufu kama Meshack, anayekabiliwa na kesi ya mauaji, amewasilisha ombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akitaka kuonana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo.

Mshtakiwa huyo anataka kuonana Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ferdnadri Kiwonde ili aweze kumuelezea changamoto zinazomkabili kutokana na upelelezi wa shauri lake kutokukamilika.

Luongo anakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mkewe aitwaye, Naomi Marijani na inadaiwa kuwa baada ya kumuuua alimchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Mshtakiwa huyo ametoa maombi hayo leo, Desemba 29, 2022, wakati kesi yake ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Amewasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga, muda mfupi baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri lake bado haujakamilika.

Kabla ya kuwasilisha ombi hilo, wakili wa Serikali, Faraja Ngukah amedai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Upande wa mashtaka baada ya kueleza hayo, mshtakiwa ambaye alikuwa anasikikiza kesi take kwa njia ya video kutoka gereza la Segerea, alinyoosha mkono juu akiashiria kuwa anataka amepewe nafasi ya kuongea.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza, mshtakiwa huyo alimuomba hakimu amsaidie ili aweze kuonana na Hakimu Mfawidhi na sehemu ya maelezo yake yalikuwa kama ifuatavyo.

“Mheshimiwa hakimu shida yangu kubwa nataka unisaidie ili nionane na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hii, nina vitu vingi vya kuongea nae kuhusiana na kesi yangu.

“Mheshimiwa hakimu tangu nifunguliwe kesi hii mpya mahakamani hapa, upelelezi wa shauri hili umekuwa haukamiliki.

“Na hata nikitaka kuzungumza kuhusu kesi hii hapo mahakamani, upande wa mashtaka wanadai kuwa nina wakili wangu yeye ndio anatakiwa azungumze kwa niaba yangu, sasa mimi nakuomba Mheshimiwa unisaidie ili niweze kuonana na Mfawidhi wa Mahakama hii (Hakimu Mkazi Mfawidhi,” amedai Mshtakiwa.

Hakimu Ngimilanga baada ya kusikiliza maombi ya mshtakiwa huyo amemshauri Luongo kuandika barua ya kuomba kuonana na Hakimu Mfawidhi.

Hakimu Ngimilanga amesema kama mshtakiwa anashida yoyote aandike barua kwa wakili wake ili aiwasilishe mahakamani hapo kwa hakimu husika.

“Mimi sina uwezo wa kukusaidia, isipokuwa utaratibu upo wazi, unatakiwa uandika barua ya kuomba kuonana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu na yeye atakapoipata atatoa maelezo ya kuonana na wewe, sawa? Amesema Hakimu Ngimilanga na kuongeza:

“Pia, kesi yako ni ya mauaji, hivyo Mahakama hii haina Mamlaka ya kusikiliza hii isipokuwa hadi upelelezi utakapokamilika siku unasomewa maelezo ya mashahidi na vilelelezo (Commital Proceedings),” amesema Hakimu. 

Hakimu Ngamilanga baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 13, 2023 itakapoitwa na mshtakiwa yupo rumande kutokana na kesi ya mauaji inayomkabili haina dhamana kwa kujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya mauaji namba 5/2022.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole, wilaya ya Kigamboni, ambapo alimuua mkewe aitwaye Naomi Marijani.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 24, 2022 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) alimfutia shtaka mshtakiwa huyo na kisha kufungulia kesi nyingine yenye shtaka hilo hilo. 

Huo ni utaratibu wa kawaida kwa upande wa mashtaka kufuta kesi na kumfungulia nyingine iwapo watabaini kuna kasoro za kisheria katika kesi hiyo.

Chanzo: Mwananchi