Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kuua kwa risasi Himo apandishwa kizimbani

Mfanyabiashara Pic Anayedaiwa kuua kwa risasi Himo apandishwa kizimbani

Tue, 6 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Hatimaye mfanyabiashara maarufu wa Mji wa mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Kennedy Minja (47) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi leo Juni 6, 2023 akikabiliwa na shtaka la kuua kwa kukusudia.

Hatua hiyo imekuja baada ya mfanyabiashara huyo kusota mahabusu kwa siku 20 tangu ajisalimishe Kituo Kikuu cha Polisi Mjini Moshi, Mei 17 mwaka huu.

Awali, akisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Philbert Mashurano mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Erasto Philly aliieleza mahakama hiyo kuwa mnamo Mei 17 mwaka huu, mfanyabiashara huyo akiwa eneo la Makuyuni, Barabara ya Himo-Marangu alimuua Deogratius Lyimo, mkazi wa Kilema.

Hata hivyo, Hakimu Philly alimweleza mshitakiwa huyo kuwa, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hapaswi kujibu chochote na kwamba shitaka hilo halina dhamana.

"Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili na hupaswi kujibu chochote mbele ya mahakama hii na shauri hili halina dhamana, upande wa mashtaka ukimaliza upelelezi wake wataendelea na shauri hili," amesema.

Hivyo baada ya kusomewa shitaka hilo, Mwendesha mashtaka huyo wa Serikali, alimwomba Hakimu Philly kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kuja kutajwa kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, Hakimu Philly aliahirisha kesi hiyo mpaka Juni 20, mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa ambapo mshitakiwa huyo alipelekwa magereza.

Mei 17, mwaka huu inadaiwa kulitokea kuzozana kati ya mfanyabiashara huyo pamoja na marehemu baada ya mfanyabiashara huyo kuingia barabarani bila tahadhari na kutaka kuwagonga wakiwa kwenye pikipiki marehemu pamoja na rafiki yake aliyekuwa naye katika Barabara ya Himo-Marangu.

Kulingana na maelezo aliyopewa baba mkubwa wa marehemu, Isaack Lyimo alieleza kuwa, katika mabishano hayo walifikia hatua ya kutaka kupigana, ndipo mfanyabiashara huyo alikwenda kwenye gari na kuchukua bastola na kumfyatulia risasi kijana huyo na kudaiwa kumuua papo hapo.

Chanzo: Mwananchi