Serikali imesema bado inaendelea na majadiliano na mshtakiwa Rhoda Salum (48), anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 23.84 za dawa za kulevya aina ya mirungi.
April mwaka huu, Rhoda, alimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kukiri shtaka lake na kupunguziwa adhabu ili aweze kuimaliza kesi hiyo.
Hata hivyo leo, Novemba 15, 2023 Wakili wa Serikali Frank Michael ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na majadiliano.
Wakili Michael ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Rubiroga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Alidai kuwa kutokana na Hakimu anayesikiliza shauri hilo kuwa na majukumu mengine ya kikazi, anaomba mahakama ipange tarehe nyingine.
Kutokana na hali hiyo, wakili wa mshtakiwa Mwesigwa Muhingo alikubaliana na upande wa mashtaka, kesi hiyo iahirishwe ili tarehe ijayo iweze kupangiwa tena muda wa majadiliano.
Hakimu Ruboroga baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 27, 2023 itakapotajwa na mshtakiwa yupo rumande.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa katika mahakama hapo, Februari 16, 2023 na kusomewa kesi inayomkabili.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 26, 2023 katika Mtaa wa Wailes uliopo wilayani Temeke.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kilo 23 za Mirungi, kinyume cha sheria.