Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kumuua mkewe kwa kumchoma moto ahoji jalada kuchapishwa miezi mitano

96934 Pic+naomi Anayedaiwa kumuua mkewe kwa kumchoma moto ahoji jalada kuchapishwa miezi mitano

Wed, 26 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hamisi Said Luonga anayekabiliwa tuhuma za mauaji ya mke wake, Naomi MarijanI ameutaka  upande wa mashtaka kukamilisha uchapishwaji wa jalada kwa haraka ili ajue hatma ya kesi hiyo inayomkabili.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Faraji Nguka kudai hayo leo Jumatatu Februari 24, 2020 mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Vicky Mwaikambo kuwa jalada lipo kwenye uchapishwaji na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

"Uchunguzi unaendelea, tunaweza tukakuambia jalada lipo  kwenye uchapaji ni kama uchunguzi wa ndani unaendelea na tupo kwenye hatua za mwisho za upelelezi," amedai Nguka.

Baada ya maelezo hayo, Luonga alinyoosha mkono na kuieleza mahakama hiyo kuwa  imefika miezi mitano sasa shauri hilo linapokuja mahakamani hapo upande wa mashtaka umekuwa ukidai jalada lipo kwenye hatua ya uchapishaji.

"Je hili faili lina ukubwa gani hadi sasa ni miezi mitano faili halijakamilika hivyo naomba mambo haya yaende haraka ili nijue hatma yangu kama mambo yalishatokea na leo hii nipo mahakamani najua Mungu atatenda haki yake," amedai Luonga

Pia, Luonga ameieleza mahakama hiyo kuwa mwaka 2019 aliingia kwenye matatizo hayo na kusababisha mtoto wake kuishi katika mazingira magumu hivyo wasiwasi wake binti huyo haishi maisha mazuri.

Pia Soma

Advertisement

Hakimu Mwaikambo baada ya kusikiliza hayo amesema suala la mtoto wa mshtakiwa huyo kuishi katika mazingira magumu hawezi kuliongelea hivyo atamtafuta mtu wa ustawi wa jamii anayeshughulika na watoto ili aweze kumweleza hayo.

"Hata kama ukiongelea kwangu mimi sitaweza kufanya chochote hivyo nitamuomba mtu anayeshughulikia na masuala ya ustawi wa jamii ili aweze kukusikiliza na aweze kumfuatilia mtoto huyo  hadi nyumbani," amesema Mwaikambo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 9, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mshitakiwa anadaiwa kuwa Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole Kigamboni Dar es Salaam alimuua mtu anayeitwa Naomi Marajani.

Inakumbukwa kuwa Hamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake Mkuranga mkoani Pwani.

Chanzo: mwananchi.co.tz