Mahakama ya Wilaya ya Arusha imezuia kwa siku 14 dhamana ya mkazi wa Sombetini jijini Arusha, Isack Robertson Mnyagi (45), anayekabiliwa na tuhuma za shambulio la kumdhuru mwili mkewe, Jackline Mkonyi (38).
Sababu za kuzuia dhamana ya mtuhumiwa huyo ni kwa usalama wake, ikielezwa maisha yake yanaweza kuwa hatarini.
Mtuhumiwa huyo amefikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Jenipher Edward. Wakili wa Serikali Charles Kagirwa, akisoma shitaka hilo alidai mtuhumiwa alilitenda Mei 23 mwaka huu saa tano usiku.
Anatuhumiwa kumjeruhi mkewe, Jackline Mkonyi (38) kwa kumng'oa jino, kumpiga na mkanda usoni, mgongoni na maeneo mengine ya mwili na kumsababishia madhara, ikiwemo kushonwa nyuzi nane chini ya jicho.
Baada ya kumsomea kosa hilo, mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo. Upande wa Jamhuri ulieleza upelelezi umekamilika na kumsomea maelezo ya awali.
Ilidaiwa mahakamani hapo Mei 23 mwaka huu, Jackline alikuwa nyumbani na watoto wake na alisikia honi ya gari nje ya geti, alipokuwa anajiandaa kwenda kufungua, alikuta mtoto wao mkubwa ameshakwenda kufungua.
Alidai mshtakiwa alipoingia ndani hakutoa salamu kwa mke wake na badala yake alielekea chumbani na Jackline alipomfuata chumbani mtuhumiwa alimvuta hadi sebuleni na kuanza kumpiga mateke, kumpiga kwa mkanda wake wa suruali maeneo mbalimbali ya mwili wake na kumng'oa jino kwa kutumia plaizi.
Ilielezwa mtuhumiwa huyo alimpigia simu mama mkwe wake na kumueleza kuwa ajiandae kupokea mzoga wake, alimpeleka mkewe nyumbani kwao na kumtelekeza nje ya geti na yeye kutokomea kusikojulikana hadi alipokamatwa Mei 27, eneo la Himo, Kilimanjaro.
Jamhuri pia waliwasilisha maombi madogo ya kuomba mshtakiwa huyo asipewe dhamana kwa sababu ya usalama wake na usalama wa mkewe.
Wakili Kagirwa aliieleza mahakama kuwa msingi wa maombi hayo ya zuio la dhamana yanaambatana na kiapo cha Mkuu wa Upelelezi wilaya ya kipolisi Muriet.
Akijitetea mahakamani hapo kuhusu maombi hayo ya zuio la dhamana, mtuhumiwa huyo alidai hakuwahi kupata wito wa polisi na hata madai ya kutoroka siyo ya kweli na kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa na shinikizo la kisiasa.
Akitoa uamuzi wa jambo hilo hakimu Jenipher alisema mahakama imezingatia mazingira ya kesi hiyo na imekubali ombi la kuzuia dhamana kwa siku 14.