Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kumteka Dewji, aomba kufutiwa shtaka la kutakatisha fedha

82078 Mo+Dewji+pic Anayedaiwa kumteka Dewji, aomba kufutiwa shtaka la kutakatisha fedha

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakili wa utetezi , Mahfudhu Mbagwa, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuta shtaka la kutakatisha  fedha linalomkabili dereva taksi, Mousa Twaleb (46), ili mshtakiwa huyo aweze kupata dhamana.

Twaleb ambaye ni mkazi wa Tegeta na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji katika kesi ya uhujumu uchumi namba 42/2019.

Mbagwa amewasilisha ombi hilo leo Oktoba 28, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipowasilishwa kwa ajili ya kutajwa.

Amewasilisha ombi hilo baada ya wakili wa Serikali, Daisy Makakala kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na jalada halisi la kesi hiyo lipo Polisi.

Makakala baada ya kueleza hayo, wakili Mbagwa alisema anaomba shtaka la kutakatisha fedha liondolewe katika hati ya mashtaka ili mteja wake apate dhamana.

“Kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umechukua muda mrefu kukamilika, naomba upande wa mashtaka mfute shtaka la kutakatisha fedha ili mteja wangu aweze kupata dhamana,” ameomba Mbagwa.

Pia Soma

Advertisement
Akijibu ombi hilo, Wakili Makakala alisema suala la kuondoa shtaka la kutakatisha fedha ni kitu ambacho hakiwezekani.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 12, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Twaleb, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao bado hawajafikishwa mahakamani ni raia wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala na raia wanne wa Msumbiji ambao ni Henrique Simbue, Daniel Berdardo, Issac Tomu na Zacarious Junior.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg, nchini  Afrika Kusini.

Wanadaiwa kwa makusudi, walitende vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum  wilayani Kinondoni, Dar es Salaam Tanzania, Twaleb na wenzake  walimteka nyara Mohamed Dewji kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach wilayani  Kinondoni, Twaleb na wenzake  wanadaiwa walitakatisha fedha Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Chanzo: mwananchi.co.tz