Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kumpa Lukuvi rushwa akutwa na kesi ya kujibu

31119 Rukuvipic TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Mohamed Kiluwa (50) amekutwa na kesi ya kujibu katika mahakama ya Wilaya ya Ilala na ataanza kujitetea Desemba 17, 2018.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Desemba 11, 2018 na hakimu mkazi, Samuel Obasi  baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Kiluwa anakabiliwa na shtaka moja la  kutoa rushwa ya Dola za kimarekani 40,000 kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi.

Akisoma Uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao leo,  Hakimu Obasi amesema "Upande wa mashtaka ulileta mashahidi sita pamoja na vielelezo vingi ikiwemo hati za Ardhi na CD.”

Hakimu Obasi amesema amepitia ushahidi wa mashahidi hao pamoja na vielelezo na kumuona  mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi na vielelezo hivi, mahakama yangu imemkuta Kiluwa ana kesi ya kujibu, hivyo chini ya kifungu namba 231(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mshtakiwa anatakiwa kujitetea,” amesema Obasi.

Baada ya kueleza hayo wakili wa mshtakiwa, Omary Madega amedai upande wa utetezi watakuwa  na mashahidi wawili, akiwemo Kiluwa.

Awali, kabla ya hakimu kutoa uamuzi huo  upande wa mashtaka walikuwa na shahidi moja ambaye alitoa ushahidi wake dhidi ya Kiluwa.

Shahidi huyo,  Wilson Luge (39) ambaye ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Wizara ya Ardhi, amedai kuwa yeye ndio aliyeshiriki zoezi la kuhakiki na kuhesabu fedha hizo Dola za 40,000 za Marekani ambazo zilikuwa katika bahasha ya kaki, juu ya meza ya waziri Lukuvi.

Akiongozwa na mawakili kutoka Takukuru, Maghela Ndimbo akisaidiana na Nikson Shayo, Luge ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, amedai kuwa baada ya kuzihesabu fedha hizo walizianisha katika fomu maalum na kisha kuisaini fomu hiyo kama sheria inavyotaka.

Hakimu Obasi ameahirisha kesi hiyo hadi  Desemba 17,2018 itakapoendelea kwa upande wa utetezi kuanza kujitetea.

Tayari mashahidi  sita wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi dhidi ya Kiluwa, akiwemo Waziri Lukuvi.

Katika ushahidi wake  Lukuvi amedai kuwa alipigiwa simu na msiri wake kuwa kuna fedha chafu kiasi cha dola 40,000milioni za Marekani zinaletwa ofisini kwake.

Amedai fedha hizo zinapelekwa na Kiluwa  ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group and Co. Ltd na Kiluwa Free Processing Zone.

Aliieleza mahakama kuwa anatambua kuna mradi wa uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda uliopo eneo la Mlandizi , wilayani Kibaha.

Lukuvi amedai kuwa eneo hilo lina ukubwa wa ekari 1000 na kwamba mmoja wa wamiliki wa mradi huo ni mshtakiwa Kiluwa.

Amedai mshtakiwa aliomba kupimiwa viwanja 73 na kwamba  Juni na Julai, 2018 alikuwa amepatiwa hati  ya viwanja 57 huku vikibaki viwanja 16 ambavyo vilikuwa havijatolewa hati na msajili.

Alieleza kabla ya kumpa hati hizo 57, Lukuvi alitoa masharti kwa mshtakiwa huyo, kuwa viwanja hivyo viendelezwe ndani ya miaka miwili na asipofanya hivyo atanyang’anywa viwanja kwa mujibu wa sheria.

Lukuvu amedai mbali na kutoa masharti kwa Kiluwa, pia alitoa maelekezo  kwa msaidizi wake ambaye ni Kamishana wa Ardhi wa Kanda ya Dar es Salaam,  Mathew  Nhonge kuwepo na masharti ya kuendeleza eneo hilo ndani ya miaka miwili.

Hata hivyo, Lukuvi amedai kuwa Mathew hakuweka masharti katika hati hizo hali liliyosababisha Lukuvi kumtaka Kiluwa kuwasilisha hati hizo  ofisini kwake ili azikague.

Katika kesi ya msingi, Kiluwa anakabiliwa na shtaka moja la kutoa rushwa kwa Waziri Lukuvi.

Inadaiwa kuwa Julai 16, 2018  katika ofisi za waziri huyo zilizopo Magogoni, Kiluwa alitoa rushwa ya Dola 40,000 za Marekani ( Sh90 milioni).

Inadaiwa kuwa  mshtakiwa huyo alitoa fedha hizo ili asiwasilishe hati ya umiliki wa viwanja 57 vilivyopo Kitalu B Kikongo na Kitalu D Disunyara katika eneo la viwandani, Kibaha mkoani Pwani.

Soma Zaidi: Mahakama yasikiliza CD kesi ya Lukuvi

 



Chanzo: mwananchi.co.tz