Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kumfungia mtoto kabatini, kujeruhi afikishwa mahakamani

35259 Pic+mtoto Mwalimu Anitha Kimako anayedaiwa kumfungia mtoto

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mwalimu Anitha Kimako anayedaiwa kumfungia mtoto wa binti yake wa kazi kabatini kwa miezi mitano amefikishwa mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa shtaka la kushambulia mwili.

Akisomewa shtaka hilo leo Jumatatu Januari 7, 2019 mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Anold Kirekiano, mwendesha mashtaka wa Serikali,  Salome Magesa amedai Desemba 27, 2018, Anitha alimshambulia binti huyo, Neema Matimbe kwa kutumia fimbo katika eneo la Area C jijini Dodoma.

Magesa amesema kitendo hicho ni kosa la jinai kinyume cha sheria namba 241 cha makosa ya jinai.

Hata hivyo, mtuhumiwa alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Februari 7, 2019.

Hali ya binti huyo mwenye umri wa miaka 15 na mwanaye wa miezi mitano ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zinaendelea vizuri.

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa idara ya watoto katika hospitali ya mkoa wa Dodoma, Dk Muzzna Ujudi amesema mtoto huyo anaendelea

vizuri tofauti na ilivyokuwa awali, wanaweza kuruhusiwa muda wowote.

Amesema mtoto huyo alikuwa na hali mbaya kwa kuwa alikuwa na uzito chini ya kilo mbili, kwa sasa umeongezeka hadi kufikia kilo tano.

“Kwa kweli wanaendelea vizuri na kilichobaki kwa sasa ni kuwaruhusu tu na kuendelea na matibabu wakiwa nje ya hospitali lakini watatakiwa kuhudhuria kliniki kila wiki,” amesema Dk Muzzna.

Amesema mpaka sasa mtoto huyo anakula vizuri na kunyonya maziwa ya mama yake pamoja na yale ya kopo na hivyo kumfanya aendelee kuwa na afya njema.

Kuhusiana na mtoto huyo kutotoa sauti, Dk Muzzna amesema hakuweza kutoa sauti kwa sababu alikuwa amechoka pamoja na mazingira aliyokuwa anaishi lakini kwa sasa anatoa sauti za kicheko na kilio kama ilivyo kwa watoto wengine wa umri wake.

“Awali alikuwa hatoi sauti kwa sababu alikuwa amechoka na kingine yule mtoto ni mpole sana si mlizi kama ilivyo kwa watoto wengine lakini sasa hivi anatoa sauti kama kawaida,” amesema Dk Muzzna.



Chanzo: mwananchi.co.tz