Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kuchomoa bastola mbele ya RC kortini

40764 Pic+bastola Anayedaiwa kuchomoa bastola mbele ya RC kortini

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam na Moshi, Emmanuel Kisoka anayedaiwa kutoa bastola mbele ya vigogo wa Serikali mkoani Kilimanjaro amefikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Desemba 26 mwaka jana katika klabu maarufu ya Redstone, hatua chache kutoka alipokuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira na kamanda wa wa polisi mkoa huo, Hamis Issah.

Kisoka alifikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernazitha Maziku na kusomewa mashtaka yake kisha kupelekwa mahabusu gereza la Karanga baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Katika shtaka la kwanza, Kisoka ameshitakiwa pamoja na mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Josephat Talanga wakidaiwa kumjeruhi kwa chupa ya bia mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina la Mbaraka Olotu.

Wakili wa Serikali, Issack Mangunu akisaidiana na Akisa Mhando walidai mahakamani hapo kuwa, siku hiyo wakiwa klabu ya Redstone washitakiwa walimpiga Olotu na chupa sehemu mbalimbali za mwili wake na kumuumiza.

Katika shitaka la pili linalomhusu Kisoka pekee, upande wa mashitaka ulidai siku hiyo mshitakiwa alishindwa kuihifadhi mahali salama bastola yake aina ya Berreta yenye namba PX 229772.

“Mshtakiwa aliionyesha bastola hiyo kwenye mkusanyiko wa watu kinyume cha kifungu namba 61 cha sheria ya udhibiti wa silaha namba 2 ya mwaka 2015,” ulidai upande wa mashtaka.

Washitakiwa hao walikana mashitaka dhidi yao na Hakimu Maziku aliwaeleza dhamana iko wazi kwa endapo kila mmoja angekuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1.5 milioni.

Pia hakimu huyo aliwataka washtakiwa hao kuwa na barua za utambulisho na vitambulisho vinavyokubalika, masharti ambayo walishindwa kuyatimiza na kupelekwa mahabusu hadi Februari 12 wakati kesi hiyo itakapotajwa tena.



Chanzo: mwananchi.co.tz