Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amnyonga mkewe na kumuua kisa amegoma kuhamia kanisani kwake!

Ally Makame Katavi Kamanda Makame

Wed, 20 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WATU sita wameuwawa katika matukio tofauti ya kikatili likiwamo la Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi, kudaiwa kumuua mkewe kwa kumnyonga hadi kufa kwa kile kinachodaiwa kukataa kuhamia kanisa analosali mume wake.

Matukio hayo yametokea kwa nyakati tofauti ndani ya wiki moja, pamoja na tukio la bibi kumuua mjukuu na kumjeruhi mwingine kwa madai wanajisaidia ovyo, huku binti aliyehitimu darasa la saba mwaka jana, kutupa mtoto wa wiki tatu kwenye shimo la choo.

Kutokana na mauaji hayo, Jeshi Polisi Mkoa wa Simiyu, linamshikilia Katibu Mwenezi huyo, Alex Lukumambaga, kwa tuhuma za kumuua mke wake, Ernestina Bruno siku ya Jumapili ya matawi. Ernestina alizikwa alhamisi iliyopita.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Shedrack Masija, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana akiwa nyumbani kwake kata ya Ngulyati, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, wakati uchunguzi ukiendelea kutokana na kelele nyingi za wananchi kuwa amemuua mkewe.

"Tumeamua kumkamata na kumuweka ndani Katibu Mwenezi huyo, ili kuruhusu uchunguzi ufanyike. Si unajua sisi Tanzania hatuna desturi ya kuchunguza huku mtuhumiwa akiwa nje? Ndiyo maana tunamshikilia," alisema Masija.

Masija alisema mtuhumiwa anadai kuwa alimpiga na kumnyonga mkewe baada ya kukuta ameweka tawi alilotoka nalo kanisani (siku hiyo ikiwa Jumapili ya Matawi).

“Alimpiga kwa kuwa alishamzuia kwenda kusali kanisani huko na sababu ya kumzuia ni baada ya mkewe kukataa kubadili dhehebu na kuhamia anakosali yeye," alisema baadhi ya majirani ambao majina yao yamehifadhiwa, walitoa taarifa hiyo kuhusu chanzo cha mgogoro hadi kusababisha mauti.

MGANGA AMCHINJA MTOTO

Mtoto wa miaka miwili, Ivan Coloman, Mkazi wa Kijiji cha Ngumbaro, Kata ya Songu, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, anadaiwa ameuawa kwa kuchinjwa shingoni kwa panga na kisha kufichwa kwenye mfuko wa sandarusi na mtu anayedaiwa kuwa mganga wa kienyeji.

Baada ya kutekeleza ukatili huo, mtuhumiwa wa mauaji hayo, Jumanne Athuman (63), naye aliuawa muda mfupi baadaye kwa kushambuliwa na wananchi waliochukizwa na kitendo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, alisema mauaji hayo yalifanyika Aprili 18, mwaka huu, majira ya saa 8:00 mchana huko katika kijiji cha Ngumbaru.

“Ni kweli aliyemchinja mtoto na yeye ameuawa na wananchi wenye hasira. Lakini mpaka ninavyoongea, nimeshatuma kikosi kazi maalum kwenda Siha kufanya uchunguzi wa kina na waniletee majibu,”alisema

Akizungumzia tukio hilo, shuhuda wa tukio hilo Julius Gasper, ambaye ni ndugu wa marehemu, alisema yeye akiwa nyumbani, watoto wanne walikuwa wanacheza nje, lakini baada ya muda kupita wakaonekana wakiwa watatu na alipowauliza yuko wapi mwenzao, wakasema wao hawajui alipoenda.

Kwa mujibu wa Gasper, baada ya taarifa hiyo, alichukua jukumu la kuanza kufuatilia aliko mtoto huyo na alipofika kwa jirani yao (Jumanne Athuman), waliona kiatu kimoja cha mtoto huyo (Ivan), kikiwa mlangoni, huku mlango ukiwa umefungwa na damu zikichuruzika kutoka ndani.

BIBI ADAIWA KUUA MJUKUU

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linamshikilia, Tatu Moshi (45) mkazi wa Lyabukande wilayani Shinyanga, kwa tuhuma za mauaji ya mjukuu wake, Joseph Juma (4), baada ya kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumwagia maji ya moto, huku akimjeruhi mwingine mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba kwa madai wanajisaidia ovyo ndani ya nyumba.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando, alibainisha hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya asubuhi.

Alisema mwanamke huyo amekuwa na tabia ya kupiga wajukuu zake mara kwa mara, kwa madai kuwa wanatabia ya kujisaidia hovyo.

Kyando alisema katika tukio la siku hiyo, mtuhumiwa huyo alimpiga mjukuu wake sehemu mbaya za mwili na kusababisha kifo chake, huku mjukuu mwingine, Jimmy Lameck mwenyewe akijeruhiwa.

“Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga tunamshikilia mwanamke, Tatu Moshi kwa tuhuma za mauaji ya mjukuu wake, pamoja na mama mzazi wa mtoto huyu Herena Nicolaus, ambaye amekuwa akishuhudia vipigo hivyo na hatoi taarifa juu ya ukatili ambao wanafanyiwa watoto wake na bibi yao,” alisema Kyando.

“Chanzo za mauaji haya ni bibi wa watoto hawa kudai kuwa wajukuu zake wamekuwa na tabia ya kujisaidia hovyo, ndipo akaamua kuwa anawapiga, ili waache tabia hiyo na kusababisha mauaji ya mjukuu wake mmoja baada ya kumpiga vibaya na kumwagia maji ya moto,” aliongeza.

AUAWA KIKATILI

Mkazi wa Mtaa wa Mpanda Hoteli katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Marieta Thomas (90), ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wasiojulikana.

Akizungumza, mjukuu wa bibi huyo, Rosemary Titus, amesema bibi yake ameuliwa jana akiwa nyumbani kwake.

Alisema bibi yake alikuwa anaishi mwenyewe na wao walikuwa wakimpelekea mahitaji pale anapohitaji huduma.

“Nimepigiwa simu na dada yangu leo asubuhi akaniambia bibi ameuliwa, nilishtuka sana, nimekuja nimekuta wamemuua, ingawa hakuna mgogoro wowote uliokuwapo,” alisema Rosemary.

Peter Mwita, jirani wa bibi huyo, alisema alimuona bibi huyo siku moja kabla ya kifo chake na hakuwa na tatizo lolote.

“Jana jioni kabla sijaenda lindoni nilipita, alikuwa amekaa hapa nje, nikamsalimia, nashangaa kusikia ameuawa ila wachunguze labda kutakuwa na mgogoro wa kifamilia,” alisema jirani huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpanda Hoteli, Christina Ibrahimu, alikiri kutokea kwa tukio hilo baada ya kupigiwa simu na mwananchi wake na kuambiwa kwenye eneo lake yametokea mauaji ya bibi huyo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Ali Makame, alisema upelelezi wa awali unaonyesha tukio hilo linahusishwa na imani za kishirikina.

TAKWIMU MATUKIO UKATILI

Matukio hayo yametokea ikiwa ni siku chache tangu Aprili 6, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, alipotoa bungeni takwimu za matukio ya ukatili yaliyoripotiwa vituo vya polisi tangu mwaka 2019 hadi Machi mwaka huu.

Alisema matukio ya ubakaji yaliyoripotiwa kwa kipindi hicho ni 19,726 na matukio ya kulawiti ni 3,260, na kwamba kesi zilizofikishwa mahakamani ni 21,063 ambapo washtakiwa 14,278 walihukumiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live