Maria George (24) Mkazi wa Kijiji cha Marembota Kata ya Kisaka Wilayani Serengeti amenusurika kufa baada ya kukatwa sehemu mbali mbali za mwili na kusababisha kiganja kutoka chanzo wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limetokea Januari 8, 2024 saa 2 usiku nyumbani kwao na Maria ikiwa ni muda mfupi baada ya shauri lao la ndoa kuamriwa katika mahakama ya mwanzo Mugumu.
Katika shauri hilo Mtuhumiwa Isuto Mantage (36) alimfikisha Mahakamani mkewe kwa madai ya kutekeleza watoto, hata hivyo mwanamke alimkataa mahakamani kwa madai ya kumfanyia vitendo vya ukatili.
Akiongea nasi, jana Jumanne Januari 9,2024 nje ya Hospitali ya Nyerere alikolazwa majeruhi, Christina George mama mzazi wa Maria anadai baada ya kutoka mahakamani binti yake hakurudi kwake bali alifikia nyumbani kwao.
“Usiku saa mbili mwanangu alitoka nje kujisaidia ghafla nikasikia kelele za kuomba msaada kufika,nikamkuta ameanguka chini amekatwa mkono na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili,nilipiga kelele huku mtuhumiwa ambaye ni mkwe wangu akikikimbia,”amesema.
Amesema,tambo za kumuua zilianza baada ya uamzi wa mahakama wa kuamru mke akae na wanawe wawili,”alinitishia kuniua sikutilia maanani na baada ya tukio hili,alinipigia simu nikiwa hospitali kuwa kama huyo hatokufa nitakuua wewe nami nife,siko tayari kufungwa,”amesema.
Anadai wameishi miaka 10 kwa shida licha ya ndugu kumsihi aoe mwingine anadai haoni mwanamke mwingine kama huyo ndiyo maana akachukua maamuzi magumu hayo.
Akiongea na Serengeti Media Centre na Antoma Tv Online kwa njia ya simu Mantage mtuhumiwa) amekiri kumkata mke wake kwa lengo la kumuua "Mimi nilijiandaa kumuua kisha nijiue maana mpaka sasa nina pakti tano za sumu ya panya na soda,”amesema.
Amesema, kitendo cha mke wake kumkataa mahakamani wakati yeye anampenda kilimfanya achukue maamuzi hayo ili wote wakose,”kama ningekuwa na vitendea kazi nilikuwa nimuulie mahakamani kisha nami nijiue maana inaumiza sana jinsi ninavyompenda anikatae,”amesema.
Daktari wa zamu Hospitali ya Nyerere Peter Markusi amesema”tulimpokea mgonjwa majira ya saa nne usiku kutokana na majeraha aliyokuwa nayo kwenye mkono na kichwani alikuwa amepoteza damu nyingi,anaendelea na matibabu,”amesema.
Hata hivyo muda mfupi baadae amethibitisha kuwa amehamishiwa hospitali ya rufaa Mkoa wa Mara kwa matibabu zaidi ”tumempa rufaa kutokana na majeraha aliyonayo hasa mkono uliokatika unaweza kutibiwa mfupa ukafanya kazi”amesema.
Polisi Wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio na wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa.