Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyewafungia wanafunzi 14 banda la nguruwe atetewa

A6f44f70a43b4b7977633bfeddd4482f Aliyewafungia wanafunzi 14 banda la nguruwe atetewa

Mon, 30 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi mkoani Rukwa, Missana Kwangura amekiri kushindwa kumsimamisha kazi Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Matala, Revocatus Tinga, anayetuhumiwa kuwafungia wanafunzi watoro 14 kwenye chumba kimoja na nguruwe.

Alisema sababu ya kutomsimamisha kazi Ofisa Mtendaji huyo ni kukwepa kukiuka Kanuni za Utumishi wa Umma badala yake atamuhamisha kituo cha kazi.

Septemba mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda alimwagiza Kwangura kumsimamisha kazi Tinga mara moja na kuhakikisha nafasi yake inazibwa haraka kwa kumpeleka ofisa mtendaji mwingine.

Akizungumza na wanahabari mjini Sumbawanga alisema baada ya agizo hilo, aliunda timu ya wataalamu ambayo inaonesha kuwa ni kweli Tinga aliwafungia wanafunzi 14 ambao tisa kati yao ni wavulana na watano ni wasichana katika jengo wanalofugwa nguruwe.

"Ofisa Mtendaji huyo alifanya msako usiku na kuwakamata wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Matala wakiwa kwenye vibanda umiza wakiangalia video.

“Walikuwa wanafunzi 14 na aliwaadhibu kwa kuwafungia kwenye jengo la nyumba ambamo chumba kimoja walifungiwa wao na chumba kingine kilikuwa na nguruwe,” alisema

Alisema katika mazingira hayo hakutenda kosa kwa sababu aliwafungia wanafunzi kwenye chumba kimoja huku nguruwe wakiwa kwenye chumba kingine ndani ya jengo moja.

Akafafanua: “Kosa alilolifanya ni kuwafungia wanafunzi wa kike na wa kiume kwenye chumba kimoja usiku kucha. Sitamfukuza kazi ila nitamuhamishia kituo kingine cha kazi.”

Mtanda alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Swahilla kilichopo jirani na Kijiji cha Matala ambapo wananchi walimweleza kuwa adhabu hiyo ni ya kikatili.

"Adhabu aliyowapatia wanafunzi hao haikubaliki, nimeagiza asimamishwe kazi mara moja kisha akabidhiwe kwa maofisa wa polisi kwa uchunguzi na ikibainika kuwa amewatendea wanafunzi hao unyama huo, ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria,"alisisitiza.

Mtanda aliongeza: "Ni jambo lisilokubalika kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji ambaye ni mlinzi wa amani katika kijiji anafanya udhalimu huo, sisi kama serikali lazima tuchukue hatua stahiki."

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili Ofisa Mifugo Mwandamizi Mkoa wa Rukwa, Respisius Mayengo, alisema kama nguruwe hao wangekuwa na homa ya nguruwe, wanafunzi hao wangekuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa.

"Bahati nzuri mkoani kwetu hakuna ugonjwa wa homa ya nguruwe. Kitendo alichokifanya ofisa huyo hakikubaliki hata kama angewafungia kwenye banda la kuku au zizi la ngombe au wanyama wengine," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz