Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyeomba rushwa ya Sh 200milion, bado anaendelea kujadiliana na DPP

84472 Pic+dpp Aliyeomba rushwa ya Sh 200milion, bado anaendelea kujadiliana na DPP

Fri, 15 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mchunguzi Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, Cosmas Batanyita (44), ameieleza Mahakama kuwa bado anaendelea na mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

Mshtakiwa huyo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Ijumaa Novemba 15 2019, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Batanyita anakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

"Mheshimiwa hakimu, ndugu zangu wanaendelea  na mazungumzo na DPP, hivyo nasubiri majibu," amedai mshtakiwa.

Batanyita baada ya kueleza hayo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon  amedai upelelezi wa kesi hiyo upo katika hatua za mwisho kukamilika hivyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Novemba Mosi, 2019, mshtakiwa huyo aliileza mahakama hiyo kuwa ameandikia barua ya kukiri na kuomba msamaha kwa DPP.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, 2019 itakapotajwa

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 9, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Kati ya mashtaka hayo saba; mashtaka matatu ni ya kushawishi rushwa, moja la kuomba na kupokea rushwa na mashtaka matatu ni ya kutakatisha fedha.

Katika kesi ya msingi, Batanyita akiwa mwajiriwa wa Takukuru anadaiwa Februari 9, 2019 katika eneo la Upanga, alishawishi na kuomba rushwa  ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi ilivyokuwa inamkabili Husein, wakati akijua  kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea katika Ofisi ya Takukuru.

Pia, anadaiwa Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, Batanyita alijipatia dola za kimarekani (USD)  20,000 kutoka Faizal  Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz