Baada ya majadiliano ya kukiri shitaka la kusafirisha kilo 23.84 za mirungi, kati ya mshitakiwa Rhoda Salum (48) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kukwama, Serikali imeamua kumsomea hoja za awali mshtakiwa huyo.
Serikali imemsomea maelezo yake leo Februari 29, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Aprili 2023, Rhoda alimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) akiomba kukiri shitaka lake na kupunguziwa adhabu ili aweze kuimaliza kesi hiyo.
Baada ya kuandika barua hiyo, Serikali ilianza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.
Hata hivyo, leo upande wa mashitaka umedai kuwa majadiliano baina ya mshitakiwa na Serikali yameshindwa kufikiwa na hivyo wameamua kumsomea hoja za awali, ili kesi hiyo iweze kuendelea na usikilizwaji.
Akimsomea hoja za awali, Wakili wa Serikali, Eva Kassa amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na shitaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
Alidai, Januari 26, 2023, eneo la Keko Temeke, mshitakiwa huyo alikamatwa akisafirisha dawa za kulevya.
Baada ya kukamatwa, walifanya upekuzi katika nyumba ya mshitakiwa na kukuta majani yanayodhaniwa kuwa ni mirungi.
Ilidaiwa kuwa baada ya kukutwa na majani hayo, Polisi waliandaa hati ya upekuzi huku ikishuhudiwa na mshitakiwa mwenyewe, shahidi huru na polisi.
Baada ya upekuzi huo, mshitakiwa alipelekwa ofisi ya Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa mahojiano ambapo alikiri kutenda kosa hilo.
Ilidaiwa kuwa, majani hayo yalipokelewa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, yalibainika ni dawa za kulevya aina ya mirungi kilogramu 23.84.
Ilidaiwa kwamba, mshitakiwa baada ya alifikishwa mahakamani hapo na kufunguliwa kesi ya kusafirisha dawa za kulevya.
Mshitakiwa baada ya kusomwa maelezo hayo, aliyakana isipokuwa majina, anwani yake, kukamatwa na Polisi na kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, Serikali haijaweka wazi idadi ya mashahidi na wala vielelezo vitakavyotumika dhidi ya mshitakiwa huyo.
Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo hayo, amepanga Machi Mosi, 2024 kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashitaka.