Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyenusurika tukio la mauaji, asimulia mshale ulivyomuingia mwilini na kukaa nao usiku kucha

69451 Pic+risasi

Fri, 2 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Nilikesha na mshale mguuni, kila ukijitikisa maumivu yanaongezeka usiku ulikuwa mrefu, kelele siwezi kupiga kwa kuwa sikujua aliyetushambulia atakuwa wapi,” anasumulia Juma Joseph (58) mkazi wa Kijiji cha Kwitete Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Joseph ambaye amelazwa wodi ya wanaume katika hospitali Teule ya Nyerere wilayani hapa akiuguza kidonda baada ya kufanyiwa upasuaji na kutolewa mshale aliochomwa na mtoto wa mpenzi wake kutokana na vurugu zilizoibika kwenye hafla ndogo nyumbani kwao, chanzo ikidaiwa ni kumnyima bia.

Katika tukio ambalo ilishuhudiwa mtu mmoja ambaye aliongozana na mdogo wa Joseph, kutoka Nyamongo wilayani ya Tarime, akiuawa na mwingine kuchomwa mshale wa makalio.

Tukio hilo lielezewa kutokea katika mazingira ambayo hayakutegemewa na kila mtu.

Ilivyokuwa

Huku akiugulia maumivu, Joseph anasema baada ya kuachana na mke wake aliyezaa naye watoto watano kutokana na kukithiri kwa migogoro katika ndoa yao, alimpata mwanamke mwingine mjane ambaye alikuwa na watoto sita, wakaamua kuishi kama wapenzi ambao anasema walifikia kuwa kama mume na mke.

Pia Soma

“Tangu mwaka 1997 nimekuwepo hapo na kuzaa naye watoto watatu, watoto wake walinichukulia kama baba mlezi. Nimepotezana na ndugu zangu siku nyingi maana nyumbani usukumani niliondoka muda mrefu na kwa muda wote huo naishi huku (Kwitete),” anasema. Anasema Julai 28, mwaka huu, mdogo wake kutoka Nyamongo, Tarime akiongozana na rafiki yake, walifika kuwasalimia nyumbani hapo ikabidi waandae hafla ndogo wakishirikisha majirani, kuonyesha furaha ya kukutana tena na ndugu yake aliyepotezana naye kwa muda mrefu ingawa hakuweka wazi ni miaka mingapi ilipita kabla ya kukutana tena.

“Tulinunua kreti ya bia, wakati chakula kinaandaliwa tukawa tunakunywa, hata muda wa utambulisho ulikuwa haujawadia maana hatukuwa na haraka kwa kuwa walikuwa wanalala sio wakuondoka. Kijana mkubwa wa mke wangu (akimaanisha mpenzi wake) ambaye ndiye mtuhumiwa naye alikuwepo akipata vinywaji pamoja nasi,” anabainisha.

Joseph ambaye wenyeji wa kijiji hicho na vijiji vya jirani wamezoea kumwita kwa utani ‘Msukuma Mtwali’ (msukuma aliyeolewa na mwanamke) anadai kuwa kijana huyo, Matinde Mkirya baada ya kumaliza bia alitaka apewe nyingine, hata hivyo walimnyima kwa maelezo kuwa zilizobaki ni za wageni, majibu ambayo yalionekana kumchukiza.

“Alisikika akisema naona wasukuma mnataka kutawala mji huu baada ya baba kufa, ngoja nije, akaingia ndani, alipotoka ghafla akaanza kushambulia kwa mshale akampiga tumboni yule rafiki wa mdogo wangu, akaanguka, mzee mmoja jirani akapigwa mshale wa makalio, nikaamua kwenda kumdhibiti akanipiga kisigino nikaanguka chini,” anasema.

Anasema hali ilichafuka, kijana huyo alikuwa akifyatua mishale ovyo, watu wakataharuki, ikawa ni kelele tu na wengine kukimbia kila mmoja akihangaika kuokoa roho yake.

Majeruhi huyo anasema yeye aliamua kujivuta chini kwa chini huku mshale ukiwa karibu na kisigino hadi alipotoka eneo hilo akasimama na kuchechemea hadi katika kichaka kilichopo karibu na barabara.

“Muda wote nilikuwa na hofu ya kushambuliwa, sikuweza kupata usingizi kwa sababu ya maumivu na hofu kwa ujumla niliwaza mambo mengi sana usiku huo, niliwakumbuka wanangu niliowaacha, hata hivyo, licha ya kutopata usingizi lakini sikuhisi njaa,” anasema.

Hata hivyo, hajui akitoka hospitali ataelekea wapi kwa kuwa hakuna mtu yeyote mpaka jana aliyefika hospitalini hapo kumjulia hali wala kumpelekea chakula, na taarifa alizonazo ni kuwa mpenzi wake ameondoka nyumbani hapo na kukimbilia kusikojulikana hukuakiacha maiti ya mgeni wao aliyefariki katika tukio hilo.

Jirani asimulia

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anadai kuwa Joseph hujishughulisha na uganga wa kienyeji na kwamba siku hiyo walifika watu waliokuwa wanahitaji huduma za matambiko akanunua bia na akataka kuchinja mbuzi wa familia hiyo.

“Mgogoro uliibuka alipotaka kuchinja mbuzi wa familia hiyo kwa ajili ya matambiko yake ya uganga ndipo kijana Mkirya (20) akiwa ameshakunywa na kulewa pombe, alichachamaa kuwa mali hizo si za wasukuma bali za baba yake, akatoka kwa hasira na kuingia ndani alipotoka alikuwa na upinde ghafla akaanza kuwashambulia na kusababisha mauaji ya mgeni mmoja na kujeruhi watu wawili kisha akatokomea,” anadai.

Anasema kitendo cha Joseph kuishi hapo kilikuwa hakimfurahishi Mkirya ambaye alikuwa akizungumza mbele ya wenzake mara kwa mara kuwa (Joseph) amefikia hatua ya kutaka kutumia mali zao walizoachiwa na baba yao kama zake wakati naye ana familia yake.

Katibu wa hospitali Teule ya Nyerere, Mboha Kazare anasema majeruhi huyo anaendelea na matibabu ya kidonda,” alifanyiwa upasuaji wa mguu kutoa chuma kilichokuwa ndani ya mguu wake wakulia.”

Kauli ya Polisi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara Juma Ndaki anasema wanamsaka mtuhumiwa huyo, ”naomba wananchi watoe ushirikiano kwa polisi ili akamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola kujibu makosa yanayomkabili.”

Aidha, aliiomba jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi pale yanapotokea matukio mbalimbali na badala yake wavitumie vyombo vyenye mamlaka ya kukabiliana na uharifu na kutoa haki ili waweze kupata haki zao.

Mbali na hilo, Kamanda Ndaki pia aliitaka jamii hususani wanaome wenye familia kutotelekeza familia zao na kukimbilia kwa wanawake wengine kwani kufanya hivyo hakujengi jamii.

“Hata kama kunaibuka migogoro katika familia ni vyema kujitahidi kuitatua kwa njia ya amani ambayo haitawasababishia watoto kupata matatizo hasa kwa ndoa kuvunjika na wao kujikuta wakilelewa na mzazi mmoja kwa shida na tabu nyingi” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz