Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyemuua mlinzi wa Kiwanda Mufindi ahukumiwa kunyongwa

Hukumu Pc Data Aliyemuua mlinzi wa Kiwanda Mufindi ahukumiwa kunyongwa

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi Wilayani Mufindi imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, mkazi wa Mafinga, Rajabu Kangarawe (32) baada ya kukutwa na hatia ya kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya Batista Uhakula aliyekuwa mlinzi wa kiwanda cha African Hardwood Limited.

Katika shauri hilo washtakiwa walikuwa wawili, huku mshitakiwa mwingine Simon Lunocho Chongolo (41) akiachiwa huru baada ya upande wa Mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa lake.

Akisoma hukumu hiyo leo Jumanne 31, 2023 Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Iringa iliyoketi wilayani hapa, Ilvin Mgeta amesema mnamo FebruarI 13, 2022 katika kijiji cha nyololo yalitokea mauaji ya mlinzi na wizi wa vitu mbalimbali ikiwemo motor katika Kiwanda cha African Hardwood Limited.

Maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo kwa pande zote mbili, Jaji Mgeta amesema ushahidi wa kimazingira umemtia hatiani mshitakiwa wa kwanza (Rajabu) baada ya kukutwa na mali na vitu mbalimbali vilivyoibiwa zikiwemo motor tatu ambazo zilitambuliwa na mmiliki wa Kiwanda hicho.

Pia, Jaji Mgeta amesema mshitakiwa huyo ametiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia ambayo ni kinyume na kifungu 196 cha kanuni ya adhabu na kuhukumiwa kunyongwa mpaka kufa kwa mujibu wa kifungu 197 cha kanuni ya adhabu sura 16 rejeo la mwaka 2022.

Naye mwendesha mashtaka wa Serikali, Yahaya Misango kabla ya hukumu hiyo kutolewa alisema kuwa adhabu ya kosa ambalo mshtakiwa ametiwa hatiani inapatikana katika kifungu 197 cha kanunu ya adhabu sura ya 16 ambapo adhabu yake ni kunyongwa mpaka kufa na haina adhabu mbadala wa kosa hilo.

"kimsingi upande wa mashtaka unaiomba Mahakama yako ijielekeze katika kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 katika kutoa adhabu kwa mshtakiwa ambaye amekutwa na hatia kama hiyo" alisema Misango

Kesi hiyo ilisimamiwa na mawakili watano ambapo kati yao, watatu wakiwa wa upande wa utetezi na wawili wa Jamuhuri.

Shauri hilo la mauaji ya kukusudia lenye namba 97/2022 lilihusisha pia mashahidi saba wa upande wa mashtaka na wawili wa utetezi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live