Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyemuua mama yake atupwa jela miaka 10

Jela Huru Huru.png Aliyemuua mama yake atupwa jela miaka 10

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemuhukumu kifungo cha miaka 10 jela, Patrick Mmasi (26), baada ya kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia mama yake mzazi, Ruth Mmasi.

Patrick alimuua mama yake kwa kumtoboa shingo kwa rato kisha kumvunja shingo na kuutupa mwili wa mama yake ndani ya shimo la maji taka la nyumba yao baada kusikia honi ya gari, nyumbani kwao Njiro jijini hapa.

Ruth alipotea tangu Desemba 11, 2021 hadi mwili wake ulipokutwa katika shimo hilo Desemba 27, 2021, ukiwa umefunikwa na shuka na mifuko ya plastiki ya kuweka mbolea.

Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Jaji Angaza Mwipopo aliyesikiliza kesi hiyo ya mauaji namba 164/2022 amapo amesema ametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa wengine.

Amesema Mahakama imemtia hatiani Patrick baada ya kupitia hoja za pande zote ambapo upande wa mashtaka wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka yanayomkabili mshtakiwa huyo, walileta mashahidi 14 na utetezi wa Patrick aliyejitetea mwenyewe bila kuwa na kielelezo chochote mahakamani.

Jaji Mwipopo amesema ushahidi wa mazingira umeonyesha Patrick ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu na kwa mujibu wa shahidi wa 3,4,7,8,10 na 11, walieleza kwa nyakati tofauti mahakamani hapo Patrick alikiri kumuua mama yake na alikwenda nao nyumbani kuonyesha mahali alipoficha rato, nyundo na simu ya mama yake aliyokuwa ameitupa kwenye shimo hilo. 

"Mshtakiwa kabla na baada ya tukio hakuonyesha anajutia yale aliyoyafanya, alijaribu kuzuia damu isitoke shingoni kwa kumfunga shuka lakini aliposikia honi ya gari akachukua shuka zilizokuwa kwenye kamba akamfunga na kumtupa kwenye shimo la maji taka," amesema Jaji Mwipopo.

Jaji huyo amesema mshtakiwa huyo aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji na baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama iliona ameua bila kukusudia na mwili ulionyesha umechomwa shingoni upande wa kulia na kitu chenye ncha kali, hivyo hakikuwa kifo cha kawaida.

"Marehemu alikuwa na majeraha mawili shingoni tukio lile ni baya na ni mbaya zaidi kulifanya kwa mama yako mzazi, mwanaume hatakiwi  kumpiga mwanamke kwa namna yoyote, nampa adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela," alieleza.

Akisoma mwenendo wa kesi hiyo ikiwemo mashahidi wa Jamhuri ambao ni Polisi na ndugu wa marehemu, alisema mashahidi hao walieleza mshtakiwa huyo alikiri kumuua mama huyo,  baada ya mama yake kumrushia nyundo, ambapo aliikwepa kisha akamfuata  na rato ambapo wakati mama yake akirudi kunyumenyume alijikwaa kwenye kabati kisha akaanguka ndipo yeye akimchoma shongoni.

Jaji aliendelea kusema kwenye maelezo hayo, alikiri alichukua simu ya mama yake nyekundu aina ya tecno kisha akaitupa kwenye shimo la maji taka ambapo aliwaongoza Polisi mpaka nyumbani hapo kisha vitu hivyo vikapatikana.

"Ushahidi wa shahidi wa pili ambaye ni daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu unaonyesha kuwa  kifo cha marehemu kilitokana na kukabwa shingo, kukosa hewa na alikuwa na jeraha shingoni na kupelekea shingo kuvunjika.Na daktari alisema jeraha  hawezi kusema alikufa kwa kutoka damu nyingi kwani mwili wa marehemu tayari ulikuwa umeshakaa muda mrefu kabla ya kufanyiwa uchunguzi huo," alieleza.

"Msimamo wa kisheria mauaji yanapotokea kwenye mazingira ya ugomvi nia ovu inakuwa haipo, hivyo mahakama inamtia hatiani Patrick Mmasi kwa mauaji bila kukusudia," alisema. 

Baada ya Mahakama kumtia hatiani kwa kosa hilo Wakili wa Serikali, Eunice Makala aliiomba Mahakama impe Patrick adhabu kali iwe fundisho kwa watu wengine wanaojichukulia majukumu ya kuondoa uhai wa watu wengine,  na kuwa marehemu alikuwa akitegemewa na watoto wawili akiwemo Patrick mwenyewe.

 Wakili wa utetezi, Peter Madeleka aliiomba Mahakama impe mteja wake adhabu ndogo kwani hana rekodi ya uhalifu hata ya kifungo cha miezi sita ili ajifunze  na kujutia kosa alilofanya.

Awali, akisoma mwenendo wa shauri hilo, Jai Mwipopo, alisoma utetezi wa Patrick alioutoa mahakamani hapo mara baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu ambaye mbali ya kukana kuishi kwenye nyumba hiyo na mama yake, lakini pia alisema hakuna shahidi aliyeieleza Mahakama kuwa alimuona akimuua.

Patrick katika utetezi wake alisema Desemba 24, 2021 alijikuta akiwa kituo cha polisi, akiteswa na kulazimishwa akubali kumuua marehemu na kudai Desemba 27,2021 akiwa kituoni ndipo aliposikia kwa mara ya kwanza kuwa mama yake amefariki.

Jaji aliendelea kueleza katika ushahidi wa Patrick alidai hakuwaongoza Polisi kwenda nyumbani kwa mama yake wala hakuwepo wakati mwili wa marehemu unapatikana, wala nyundo, rato na simu kama ilivyodaiwa na baadhi ya mashahidi mahakamani hapo.

Baada ya uamuzi huo uliosomwa kwa zaidi ya saa mbili, Wakili Madeleka alieleza waandishi wa habari nje ya Mahakama kuwa hawajaridhika na uamuzi huo na wanatarajia kukata rufaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live