Mahakama Kuu ya Tanzania, imemhukumu adhabu ya kifo, Erick Thomas kwa jina maarufu ‘Mremi’ baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa makusudi baba yake mzazi, Thomas Mremi (80) na kisha kumzika pembeni ya nyumba yao.
Maiti ya mzee huyo iligunduliwa na kaka wa marehemu, Richard Mremi ambaye alisafiri kutoka Moshi hadi Sumbawanga baada ya taarifa kuwa kaka yao haonekani nyumbani kwake, lakini ndani ya nyumba akabaini kisu chenye damu kilichomtoa mashaka.
Hukumu dhidi ya Erick Thomas imetolewa leo Aprili 17, 2024 na Jaji Deo John Nangela wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, ambaye katika hukumu hiyo ameanza kwa kunukuu mstari wa Biblia “Na watoto watawashambulia wazazi wao, na kuwafisha”.
Jaji amesema kwa masikitiko, mshtakiwa aliamua kutimiza maandiko hayo kwa kumuua baba yake mzazi katika tukio ambalo tarehe hasa ya mauaji haijulikani, lakini ilikuwa mwezi Julai 2021 katika eneo la Kantalamba Mazoezi, Manispaa ya Sumbawanga.
Akichambua maelezo ya upande wa mashtaka juu ya kosa hilo, Jaji amesema mshtakiwa na baba yake, walikuwa wakiishi pamoja katika eneo hilo la Kantalamba Mazoezi na Desemba 2020 walipokea wageni wawili.
Wageni hao walikuwa ni Richard Mremi na John Mremi ambao ni wadogo zake na marehemu, ambao walikaa kwa siku tatu na kuondoka kwenda Moshi pamoja na kaka yao ambaye sasa ni marehemu, ambaye alikaa kwa muda mrefu huko Moshi.
Akiwa Moshi, marehemu aliwaambia wadogo zake kuwa mtoto wake ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji, amekuwa akimpiga na kumfanyia vitendo visivyo vya kibinadamu, ambapo ndugu hao walimpigia Erick na kumuonya juu ya tabia hiyo.
Muda wa mzee Thomas Mremi kukaa Moshi ukamalizika na hivyo kuhitajika kurudi Sumbawanga lakini kwa kuwa wadogo zake walihitaji kufahamu kama amefika salama na kwa vile hana simu, walimpigia mwenyekiti wa mtaa, Kyandwike Mwaipopo.
Ingawa wakati Kyandwike anapigiwa simu alikuwa safari, lakini aliporudi alikwenda moja kwa moja kwa Mzee Thomas na kumkuta mshtakiwa na alipomuuliza mzee Thomas yuko wapi, alimjibu kuwa baba yake tangu aende Moshi alikuwa hajarejea Sumbawanga.
Mwenyekiti huyo alirudisha majibu kwa wadogo wa mzee huyo huko Moshi na hilo liliwatia wasiwasi, ambapo mdogo wa marehemu aitwaye Richard Mremi akaamua kusafiri Julai 27, 2021 kwenda Sumbawanga ili kutafuta ukweli wa mahali alipo kaka yake.
Baada ya kufika Sumbawanga, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Sumbawanga juu ya kutoweka kwa kaka yake na kisha akarudi nyumbani kwa kaka yake ambako alimkuta mshtakiwa na kumuuliza alipo baba yake, akamjibu kuwa amesafiri kwenda Moshi.
Mwili ulivyogundulika
Bila kuchoka na akiwa amekanganyikiwa akiwa hajui nini kimempata kaka yake, Richard akatilia mashaka kisu kilichokuwepo ndani ya nyumba, ambacho kilionekana kama kina matone ya damu, akaamua kukagua mazingira ya nyumba.
Katika kuchunguza mazingira yanayozunguka nyumba ya marehemu, aliona eneo nyuma ya nyumba likiwa na dalili kuwa lilichimbwa na kutengenezwa tuta na juu yake kulikuwa na majivu kama vile kuna mtu alikuwa anachoma takataka juu ya tuta lile.
Kwa vile kulikuwa pia na nzi wanarukaruka katika eneo hilo, udadisi wake uliongezeka akaamua kutafuta jembe ili kuondoa udongo wa juu na alipokuwa akiendelea kufukua, alikutana na harufu mbaya kama vile kuna mtu alikuwa amezikwa katika eneo lile.
“Bila kuchelewa, Richard alimjulisha Mwenyekiti wa mtaa Kyandwike na alipofika pale na kushuhudia kile Richard alichokiona, alipeleka mara moja taarifa Polisi Sumbawanga na maofisa wa Polisi walifika mara moja katika eneo la tukio,”alisema Jaji Nangela.
Mwili ule ulifukuliwa na kubainika ni wa Mzee Thomas na ili kubaini sababu za kifo, mwili ulipelekwa Kituo cha Afya Mazwi ambapo Dk Mussa Mbalamwezi aliuchunguza na kubaini ilisababishwa na kuvunja damu ndani na nje ya mwili huo.
Hiyo kwa mujibu wa Dk Mbalamwezi, ilisababishwa na majeraha yaliyokuwepo katika kifua na tumboni yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali na hapo mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa kwa mlinzi wa amani na kukiri yeye ndiye aliyemuua.
Mshtakiwa alivyojitetea kortini
Katika utetezi wake baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu, mshtakiwa alianza kwa kukiri kuwa ni kweli alikuwa akiishi na baba yake na alikuwa na uhusiano mzuri na baba yake muda wote wakiishi pamoja na yeye ndiye alikuwa akimtunza.
Aliieleza mahakama alikamatwa Julai 29, 2021 na kuwekwa mahabusu na baadaye kutolewa kwa ajili ya kuandika maelezo yake ya onyo na kwamba kukamatwa kwake kulitokana na kutoonekana kwa baba yake Moshi wala nyumbani Sumbawanga.
Baaadaye, alisema alishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi baba yake kosa ambalo alilikanusha.
Alieleza kuwa alisikiliza ushahidi wa baba yake mdogo (Richard) na kwamba hakusema ukweli bali anamtuhumu tu kumuua kaka yake wakati si kweli.
Pia akasema alisikiliza ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni mlinzi wa amani na kuwa kile alichokieleza, alikieleza akiwa katika shinikizo la maofisa wawili wa Polisi na hivyo hakukiri bali ilikuwa ni shinikizo na akakanusha kutenda kosa hilo.
Katika maswali ya dodoso, mshtakiwa alikanusha kumuua na kumzika baba yake nyuma ya nyumba, lakini akakiri kuwa kwa vile ni yeye tu ndio alikuwa akiishi na marehemu, basi ilikuwa sahihi kwa polisi kumuhoji kuhusu mahali alipo baba yake huyo.
Adhabu ya kifo
Jaji Nangela katika hukumu yake alisema hakuna ubishi kuwa mzee Thomas ni marehemu na kifo chake sio cha kawaida na ushahidi wa mashahidi wa kwanza hadi wa nne wa mashtaka ulikuwa ni mzito na muhimu kwa upande wa mashtaka.
“Mathalan, shahidi wa Richard na Kyandwike ambao ndio watu wa kwanza kufuatilia kutoweka kwa Mzee Thomas walieleza ufuatiliaji walioufanya hadi kupatikana kwa mwili wake ukiwa umezikwa nyuma ya nyumba yake walikokuwa wakiishi na Erick,” alisema.
“Shahidi wa kwanza (Richard) alikuwa shahidi muhimu ambaye alikuwa na kaka yake hukoMoshi hadi aliposafiri kurudi Sumbawanga alipokutana na kifo cha uchungu na cha kikatili. Mshtakiwa alipohojiwa ya Richard na Kyandwike alikiri kumuua,” alieleza.
“Chini ya kifungu cha 27 cha sheria ya ushahidi kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, aina hiyo ya kukiri kosa inakubalika kisheria. Lakini hakuishia hapo tu kwani alikwenda na kukiri hilo mbele ya mlinzi wa amani (Yusuph Daud Sakala,”alisema Jaji.
“Kama shahidi wa kwanza (Richard) na wa pili, (Kyandwike) wangekuwa wamemuona mshtakiwa akiteswa wangeaimbia mahakama. Hata hivyo mshtakiwa wala hakuhoji juu ya suala hilo kwa mashahidi waliosema alikiri kutenda kosa hilo la mauaji”
Jaji alisema anaridhika kuwa kitendo cha mshtakiwa kushindwa kuwahoji mashahidi katika kipengele cha yeye kukiri kufanya mauaji, inamaanisha alikubaliana na simulizi yao kwamba ilikuwa ni sahihi na ulikuwa ni mkweli juu ya kile alichokisema.
Katika kuthibitisha shtaka la mauaji ni lazima kuwepo ushahidi wa uwepo wa nia ovu, hivyo Jaji akasema katika kesi hiyo upande wa mashtaka ni lazima uithibitishie mahakama kuwa Erick Mremi alikuwa na utimamu wakati anatenda kosa hilo.
Jaji alisema kulingana na shahidi wa kwanza, wa pili na wa sita, mshtakiwa alisimulia mwenyewe kuwa siku ya tukio, alikuwa amemtaka baba yake ampe hati ya nyumba na alianza kudai hati hiyo kwa kumpiga kwanza baba yake kwa nondo.
Kisha baadae akampiga hadi kumuua na kwamba baadae alimfunga mikono na miguu na kumzika upande wa nyuma wa nyumba ambapo Jaji alisema matukio yote hayo yanadhihirisha mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kumaliza kabisa uhai wa baba yake.
Ni kutokana na ushahidi huo na ushahidi wa upande wa mashtaka kwa ujumla wake, anamuona mshtakiwa ana hatia na anamhukumu kunyongwa hadi kufa kwa vile upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi yake pasipo kuacha mashaka.