Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyemuibia mumewe Sh mil 198 alipa faini Sh mil 7

Ceo D . Law Aliyemuibia mumewe Sh mil 198 alipa faini Sh mil 7

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisa Utamaduni Manispaa ya Lindi, Makalaghe Shekhalaghe Mkinda (50) amelipa faini ya Sh7 milioni na kukwepa kifungo cha mwaka mmoja jela kama alivyohukumiwa.

Katika kesi ya msingi, Shekalaghe alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 122/2021 kwa kutenda kosa kati ya Januari, 2020 na Juni 2020, jijini Dar es Salaam la kuiba Sh198 milioni kutoka katika akaunti ya NMB iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu mume wake, Suleiman Mohamed.

Juni 30, 2023, Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alitoa hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh7 milioni.

Mbali na adhabu hiyo, Mahakama hiyo iliamuru nyumba yake iliyopo Msavu mkoani Morogoro ichukuliwe na kuingizwa katika mirathi namba 23 ya mwaka 2022, iliyofunguliwa Mahakama ya Mwanzo Sinza.

Hakimu Kabate alisema mashahidi wanne wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa huyo.

Akipitia ushahidi, Hakimu Kabate alisema mshtakiwa alikuwa mke wa tatu wa marehemu Mohamed na kwamba kukiri kwake katika utetezi wake na ushahidi wa taarifa za kibenki uliowasilishwa mahakamani hapo, unaifanya Mahakama isiwe na maswali ya ziada ya kujiuliza juu ya ukweli kuwa mtuhumiwa aliiba kiasi hicho cha fedha.

“Mshtakiwa mwenyewe ulikiri kutoa na kutumia fedha kwa matumizi binafsi na kutoa sadaka katika Msikiti wa Huddah mkoani Lindi, sasa sijui ulikuwa unachukua hela bila kujua ama ni kiburi? Na ulikataa hawajawahi kufungua mirathi,” alisema Hakimu.

Hakimu Kabate alisema mtoto mkubwa na marehemu, Mohamed alitoa ushahidi na kudai walishafungua mirathi lakini mshtakiwa aliendelea kutoa fedha kupitia ATM.

“Ingawa kwa macho ya watu inashangaza, unaibaje hela ya marehemu mpendwa wako? Kulikuwa kuna haja gani ya wewe kuendelea kutoa fedha? Ni kiburi au nini? Ulitakiwa uwe na subra kwa sababu mlishafungua mirathi, hivyo hapa nakutia hatiani kwa kosa la wizi wa fedha katika akaunti ya mume wako,” alisema Hakimu Kabate.

Alisema katika utetezi wa mshitakiwa alioutoa kabla ya hukumu alisema sehemu ya fedha alizoiba alizitoa kama sadaka katika msikiti na shahidi wake alieleza jinsi walivyonufaika na msaada huo, Mahakama imeona impunguzie adhabu.

“Mahakama imeshawishika na hoja za wakili wa utetezi alizozitoa kupitia kifungu cha 27(2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022, kuwa mshtakiwa ni mkosefu kwa mara ya kwanza na anaomba apewe adhabu ndogo ambayo ni kulipa faini na sio kifungo, hivyo nina wiwa kumpa adhabu ya kulipa faini” alisema Hakimu Kabate.

Hakimu Kabate alisema, amezingatia pia mshtakiwa hana kumbukumbu za makosa ya nyuma, ana familia inayomtegemea, ikiwamo watoto yatima na anamhudumia mzazi ambaye amefanyiwa upasuaji.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Agness Mtunguja na Eva Kassa, uliomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe somo na fundisho kwa mshitakiwa na jamii inayomzunguka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live