Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam imemhukumu mfanyabiashara Yohana Mwambusi (23) kifungo cha nje miezi sita, baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga ngumi na mateke mfanyabiashara mwenzake.
Pia, Mahakama hiyo, imemuamuru Mwambusi, kumlipa mlalamikaji Elizabeth Sengalawe Sh15,000 ndani ya siku 30.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi, Januari 11, 2024 na Hakimu Gladness Njau, baada ya mshtakiwa kukiri shitaka lake wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa mara ya kwanza kumsomea mshtakiwa kosa lake.
Akitoa adhabu hiyo, Hakimu Njau amesema kwa kuwa mshtakiwa amekiri kosa mwenyewe, hivyo anamhukumu kifungo cha nje miezi sita na hatakiwi kufanya kosa ndani ya kipindi hicho.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Mwambusi aliomba msamaha kwa mlalamikaji Elizabeth, kitendo cha kumpiga baada ya kutokea kutoelewana ambako mlalamikaji huyo aliieleza Mahakama kuwa yuko tayari kumsamehe.
Kwa mujibu ya hati ya mashtaka, mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 7, 2024, eneo la soko la samaki ferry lililopo wilayani Ilala.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Mwambusi alimshambulia Elizabeth Sengalawe kwa kumpiga ngumi, mateke na makofi na hivyo kupelekea kumsababishia maumivu mwilini.