Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyemlawiti mkewe kama adhabu afungwa miaka 30

Hukumu Pc Data Aliyemlawiti mkewe kama adhabu afungwa miaka 30

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, imemtia hatiani mkazi wa Kitelewasi, Dickson Mbwilo (42) na kumtupa jela miaka 30 kwa kosa la kumlawiti mkewe kama adhabu kila anapokosea.

Kulingana na maelezo ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32, mumewe alikuwa akimfanyia kitendo hicho pale anapokuwa amemkosea, ili iwe ndiyo adhabu yake, hali mbayo ilimsababishia sehemu zake siri kuharibika vibaya.

Hata hivyo, hadi Mbwilo anatiwa hatiani na kufungwa, mlalamikaji hakuwahi kufika kortini kutoa ushahidi wake, isipokuwa Mahakama iliamua kuegemea maelezo yake aliyokuwa ameyaandika polisi.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 6, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Benedict Nkomola na nakala yake kupatikana leo Machi 12, ikisema ushahidi uliotolewa umethibitisha mashtaka dhidi ya Mbwilo.

Hakimu amesema katika kesi ya jinai, maelezo ya mlalamikaji yanaweza kutumika kama sehemu ya ushahidi kwa kuwa sheria ya ushahidi inatoa utaratibu wa kushughulika na kesi ambazo mlalamikaji atakuwa hapatikani kutoa ushahidi.

Ilielezwa mahakamani kuwa baada mshtakiwa kukamatwa na Polisi na kupewa dhamana, mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni mkewe alitoweka na hajulikani alipo na hukumu inatolewa, hakuwahi kupanda kizimbani kutoa ushahidi.

Katika hukumu hiyo, Hakimu anasema kwa nyakati tofauti, mshtakiwa alitenda makosa hayo ambapo alitenda kosa la kwanza Aprili, 2021 na kurudia Mei 15, 2022 na Desemba 30, 2022, matendo ambayo ni kinyume na kifungu 154 (1) (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la Mwaka 2022.

Mshtakiwa alikuwa akimlazimisha mkewe kumwingilia kinyume na maumbile katika nyumba yao iliyopo Kata ya Rungemba, Mafinga na alikuwa akichukua uamuzi huo kama adhabu kwa mkewe pindi tu anapomkosea.

Kulingana na ushahidi huo, mwanamke huyo alishindwa kutoa taarifa kuhusu kitendo ambacho mume wake anamfanyiwa kwa sababu ya kulinda ndoa yake, lakini baada ya ndugu kumhamasisha ndipo alipoamua kutoa taarifa hiyo.

"Kutokana na kitendo ambacho alikuwa anamfanyia mkewe, aliwaambia ndugu zake ambao walimtia moyo na baadaye alienda Polisi kueleza ukatili anaofanyiwa, ndipo mshtakiwa akakamatwa Mei 19, 2022,” inaeleza hukumu hiyo.

Kuhusu utetezi, hakimu anasema mshtakiwa hakuwa na pingamizi lolote juu ya maelezo ya mkewe kupokelewa kama kielelezo cha upande wa mashtaka na hivyo maelezo hayo yalisomwa mahakamani na Polisi aliyeyaandika.

"Hakukuwa na pingamizi lolote kutoka kwa mshtakiwa juu ya maelezo ya mwathirika, ambayo aliyatoa polisi na sasa hapatikani na hajulikani alipo, hivyo Mahakama ilipokea maelezo hayo kuwa sehemu ya ushaidi kwenye kesi hiyo,” amesema Hakimu Nkomola.

Baada ya mahakama kupokea ushahidi huo na kusikiliza utetezi wa mshtakiwa, llimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Kabla ya adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Yahaya Misango aliomba mahakama impe adhabu kali ili kuzuia matukio kama hayo kwenye jamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live